HabariSiasa

Serikali yaomba mchango kujenga kituo cha saratani

July 31st, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

WANANCHI wameghadhabishwa na hatua ya serikali kuwaomba wachange fedha za ujenzi wa kituo cha matibabu ya kansa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Hospitali hiyo ilitoa wito kwa wahisani kutoa michango ya kifedha kupitia kwa M-Pesa ili kupata Sh230 milioni kwa ujenzi wa jumba la orofa tatu ambalo litakuwa makazi ya wagonjwa wa kansa wanaoendelea kupokea matibabu.

“Hatua hii inatarajiwa kuleta matokeo bora kwa matibabu ya kansa na pia kuboresha uwezo wa wagonjwa kukamilisha matibabu hasa ya “radiotherapy” na “chemotherapy,” ikasema sehemu ya ombi hilo ambalo pia limechapishwa kwenye tovuti ya KNH.

Lakini wananchi wengi wameshangaa inawezekanaaje hospitali inayosimamiwa na serikali kuu yenye bajeti ya taifa ya Sh3 trilioni, kuomba raia Sh230 milioni wakati mabilioni ya fedha yanazidi kuporwa.

Raia walitaka hospitali hiyo ielekeze ombi lake kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA), ambayo hukusanya kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwao kwa minajili ya matumizi ya serikali.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wahudumu wa Matibabu, Wafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU), Dkt Chibanzi Mwachonda alisema ombi hilo ni sawa na matusi kwa wananchi.

“KNH hufadhiliwa kwa pesa za mlipaushuru, ni shirika la kitaifa linalojikusanyia pesa na pia hupokea fedha kutoka kwa Wizara ya Fedha. Mahitaji haya yangejumuishwa kwenye bajeti ya 2019/2020. Hii ni matusi kwa walipa ushuru na Wakenya wakarimu ikizingatiwa mabilioni ambayo hupotea kwa ufisadi,” akasema.

Upekuzi hospitalini humo huwa umefichua jinsi baadhi ya wagonjwa hulazimika kulala sakafuni au hata nje kwenye baridi wakisubiri kuhudumiwa. Wengi huwa wametoka maeneo ya mbali nchini.

Miaka miwili iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alizindua kituo cha matibabu ya kansa katika hospitali hiyo akaahidi kwamba muda wa matibabu ungepungua kutoka miezi mitatu hadi mwezi mmoja.

Aliahidi kuwa serikali yake ilijitolea kikamilifu kupambana na kansa, hivyo basi ingeendelea kufadhili upanuzi wa hospitali za kitaifa kutibu magonjwa hayo.

“Serikali yangu itapanua vituo vya matibabu ya kansa katika KNH na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, Eldoret, na vilevile kufungua vituo sita vipya vya matibabu ya kansa katika maeneo mengine muhimu kote nchini,” akasema Agosti 24, 2017.

Kulingana na KNH, hitaji la kukamilisha matibabu ni mojawapo ya mbinu zinazoweza kuboresha afya ya wanaougua saratani, ambayo inazidi kusababisha maangamizi humu nchini.

Hospitali hiyo ilisema ilifanya utafiti mnamo 2016 ikapatikana karibu asilimia 30 ya wagonjwa hawakukamilisha au walichelewesha matibabu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosa fedha za matibabu, pesa za kusafiri hadi Nairobi na kugharamia makao jijini wakitibiwa, njaa na kiu, kusubiri muda mrefu kabla wahudumiwe na kukosa mahali pa kupumzika siku nzima.