Habari Mseto

Serikali yaondoa hofu kuhusu 'Huduma Namba'

February 19th, 2019 1 min read

Na WAIKWA MAINA

KATIBU wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho amesema kwamba namba mpya ya usajili wa kitaifa maarufu kama “Huduma Numba” itatumika katika mipango inayowahusu wananchi pekee.

Kumekuwa na hofu kwamba huenda nambari hiyo ikatumika katika masuala mengine, kinyume na yale yaliyoelezwa na serikali.

Akihutubu katika kijiji cha Manyatta, Olkalou, Kaunti ya Nyandarua alikozindua majaribio ya mpango huo, Dkt Kibicho alisema kwamba namba hiyo maalum itatumika kutoa habari zote muhimu kumhusu mtu binafsi, na itaisaidia sana katika mipango ya kitaifa.

Katibu huyo aliwahakikishia wakazi kwamba baadhi ya masuala makuu ambao mpango huo utaisaidia serikali ni utoaji haraka wa vitambulisho vya kitaifa, mchakato aliosema kwamba huwa unachukua hadi miezi sita.

Alisema kwamba serikali itaanza kuwasajili wananchi kabla ya kuanza Mfumo wa Kitaifa wa Kuwatambua Watu (NIIMS) ili iwe rahisi kwake kuweka majina yao katika mfumo huo.

“Mfumo huo utakuwa muhimu sana, hasa katika kuisaidia serikali kuweka mipango mbalimbali kama mahitaji ya watoto walio chini ya miaka mitano. Baadhi ya masuala hayo ni kama afya, elimu kati ya mengine,” akasema.

Alikanusha madai kwamba itamhitaji mtu kutolewa dau ili kufanyiwa utafiti wa DNA, akitaja hayo kama uvumi usio na msingi wowote.

“Ikiwa tungekuwa tukikusanya damu, basi tutaiweka wapi? Tungehitaji mabohari au mitungi mikubwa. Hakuna nchi yoyote ishawahi kufanya hivyo kote duniani. Tunachohitaji ni picha ya mtu pekee,” akasema.

Baada ya kukamilika kwa mpango huo, vifaa vya usajili vitaachiwa manaibu wa machifu ambo wataondoa majina ya watakaofariki na kuongeza majina ya watoto watakaozaliwa.

Mfumo huo pia utanakili shughuli za kiuchumi za eneo husika, ili kuisaidia serikali kupanga kuhusu masuala ya maendeleo.

Gavana Francis Kimemia alisifu mpango huo, huku akiishukuru serikali kwa kuichagua Nyandarua kama eneo la uzinduzi wake. Wakazi wengi walikuwa washajitokeza kwa wingi kufikia saa tano asubuhi.