Habari za Kitaifa

Serikali yaondoa ufadhili wa lishe shuleni licha ya kuongeza ushuru

May 15th, 2024 2 min read

NA DAVID MUCHUNGUH

MAMILIONI ya wanafunzi ambao wamekuwa wakinufaika na mpango wa lishe shuleni huenda wakakosa chakula kuanzia Julai mwaka huu, ikiwa mapendekezo katika bajeti ya 2024/2025 yatapitishwa na Bunge la Kitaifa.

Mapendekezo ya Idara ya Kitaifa ya Elimu ya Msingi ambayo yametayarishwa na Kamati ya Bajeti hayajatenga pesa zozote kwa mpango huo unaoendelea katika kaunti 26 ambazo zinachukuliwa kuwa zilizotengwa.

Mapendekezo hayo ya bajeti pia hayana ufadhili wa kutosha kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule za msingi, sekondari msingi na sekondari za umma.

Kukosa kutengea pesa mpango wa lishe kunaenda kinyume na manifesto ya Kenya Kwanza ambayo iliahidi kuongeza bajeti yake maradufu ili kuongeza idadi ya wanaonufaika kutoka milioni mbili hadi milioni nne na kutoa ruzuku kwa serikali za kaunti kupanua mpango huo.

Katika mwaka huu wa kifedha, mpango huo ulitengewa Sh4.9 bilioni.

“Inafaa kufahamika kuwa Mpango wa Lishe Shuleni haukufadhiliwa.

“Huu ukiwa mpango muhimu unaopewa umuhimu katika sekta ya elimu, tunaomba kudumishwa kwa bajeti ya Sh4.9 bilioni,” inasema barua ya Wizara ya Elimu kwa Kamati ya Idara ya Elimu na Utafiti.

Mpango wa lishe kwa kawaida huendeshwa na serikali ya kitaifa na za kaunti.

Mwaka jana, kamati ya bunge kuhusu elimu ilipendekeza Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) kushirikishwa katika mpango wa lishe shuleni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Julius Melly alisema itafuatilia suala hilo na Hazina ya Kitaifa ili kufadhili mpango huo.

Ikiwa ufadhili hautarejeshwa, utaathiri mahudhurio na kudumisha watoto shuleni miongoni mwa watu maskini kote nchini.

Pia, mpango wa Dishi na County unaoendeshwa na Kaunti ya Nairobi kupitia ushirikiano na Wizara ya Elimu utaathiriwa. Serikali ya Kaunti ilikusudia kuchangia Sh1.2 bilioni kwa kitita hicho huku Wizara ya Elimu ikitoa kiwango sawa na hicho.

Hata hivyo, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja aliambia Taifa Leo kuwa kaunti hiyo imekuwa ikiendesha mpango huo kivyake.

“Tumekuwa tukiendesha mpango huu peke yetu. Hatujapokea hata shilingi moja kutoka kwa Wizara lakini hautaisha. Ufadhili huo ni wa serikali ya kaunti na washirika wetu wa maendeleo. Hakuna mtoto anayekosa shule kwa kukosa chakula isipokuwa akiwa mgonjwa,” alisema.

Bw Sakaja alisema kuwa mpango huo umeongeza idadi ya watoto katika shule za msingi za umma Nairobi kwa asilimia 24 na kwamba kufikia mwisho wa muhula wa kwanza, ulikuwa umefaidi wanafunzi 184,000.

Muhula huu, utanufaisha wanafunzi 200,000. Wizara ya Elimu pia imepunguziwa mgao wa kufadhili elimu ya sekondari za kutwa (Sh1.5 bilioni), Elimu ya Msingi Bila Malipo (Sh1.2 bilioni) na Sh347 milioni za shughuli nyingine tofauti.