Serikali yaonya wasimamizi wa vyama vya kahawa

Serikali yaonya wasimamizi wa vyama vya kahawa

IRENE MUGO Na STEPHEN MUNYIRI

WAZIRI wa Kilimo Peter Munya ameonya kuwa bodi za vyama vya ushirika ambazo zitazuia wakulima kupata pesa za hazina ya Kahawa zitavunjwa.

Wakulima wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wasimamizi wa vyama vya ushirika wamekuwa wakiwanyima pesa kutoka hazina hiyo iliyotengewa Sh3 bilioni na serikali ya kitaifa.

Akizungumza akiwa Mathira, kaunti ya Nyeri wakati wa kupokea maoni kutoka kwa umma kuhusu mswada wa kahawa, Bw Munya alisikitika kuwa pesa hizo hazitumiwi huku wakulima wakipata mikopo ghali kutoka taasisi nyingine za kifedha.

“Tumegundua kwamba baadhi ya wakulima hawaombi pesa kutoka hazina hiyo lakini tunajua shida ni nini na tutachukua hatua,” akasema Bw Munya.

Alisema ni makosa kwa wanachama wa bodi za vyama vya ushirika kukataa kutia saini zao katika fomu ili kuwanyima wakulima haki yao ya kunufaika na pesa hizo.

“Ofisi yangu itachukua hatua na kuvunja bodi hizo kwa sababu tumegundua sababu ya wakulima kutochukua mikopo ni bodi kukataa kutia saini fomu zao, hii haikubaliki,” akaongeza Bw Munya.

Alisema pesa zilizotengewa hazina hiyo kwa lengo la kufufua sekta ya kahawa zingali benki kwa sababu wakulima hawajatuma maombi. Bw Munya alisema kwamba bodi za vyama vya ushirika zinadaganya wakulima kwamba wakikopa kutoka hazina hiyo, watakuwa wamepatia kampuni ya New Kenya Planters Cooperative Union (KPCU) haki za kusaga kahawa yao.

“Nataka kuwaambia wakulima wa kahawa kwamba propaganda inayosambazwa katika vyama vya ushirika kwamba kukopa pesa hizo kutawarudisha katika chama cha new KPCU ni uongo, hakuna anayelazimisha wakulima na wana uhuru wa kuchagua kampuni wanayotaka hata baada ya kukopa kutoka hazina hiyo,”akasema Bw Munya.

Wakulima walisema kwamba maafisa wa vyama vya ushirika wamekuwa wakishirikiana na benki kuwapa mikopo wakulima ili waweze kupata kiinua mgongo.

“Tunataka mikopo hiyo lakini maafisa wanataka tukope kutoka benki,” akasema mkulima Peter Mathenge. Bw Munya alisema kwamba wizara yake haitakubali wakulima wanyanyaswe.

“Kama wizara, hatutabaki kutazama wakulima wakipata madeni kwa sababu ya riba ya juu wakikopa pesa kutoka benki, kwa hivyo, tutachukua hatua,” alionya.

Hazina hiyo ilianzishwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa lengo la kukinga wakulima wasipate hasara baada ya kuvuna zao lao. Bw Munya waliwahimiza wakulima kuchukua mikopo kutoka hazina hiyo kwa kuwa inatoza riba ya asilimia tatu pekee.

Bw Munya alisema serikali imetenga pesa za kufufua chama cha ushirika cha wakulima wa kahawa cha Mathira North ambacho kiliporomoshwa na madeni.

You can share this post!

Tuliteua Bi Kavindu kwa misingi ya sifa za uongozi –...

FUNGUKA: ‘Jikedume mambo yote’