Serikali yaonya wimbi la tatu la corona lanukia nchini Tanzania

Serikali yaonya wimbi la tatu la corona lanukia nchini Tanzania

Na MWANANCHI

SERIKALI ya Tanzania imesema kuna ishara kwamba wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19 litatua nchini humo, na kuhimiza raia wachukue tahadhari zaidi kujikinga.

Akizungumza na waandishi wa habari mnamo Jumamosi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Mkurugenzi wa Masuala ya Kinga katika Wizara ya Afya, Dk Leonard Subi, alitoa maagizo kadhaa ikiwemo kuwataka wananchi kuvaa barakoa wakati wote.

“Wizara inawakumbusha wananchi wote kutopuuza ugonjwa wa Covid-19. Wizara imeanza kuona viashiria vya kutokea kwa wimbi la tatu la mlipuko wa ugonjwa huu katika nchi yetu,” alisema Dkt Subi.

Akaongeza: “Hii ni kutokana na taarifa za ufuatiliaji wa mwenendo wa ugonjwa huu zinazofanywa na wizara na mwingiliano kati ya watu wetu na mataifa mengine.”

Mkurugenzi huyo alihoji kuwa idadi ya wagonjwa wanaopatikana na virusi vya corona, ambavyo ndivyo vinasababishaa Covid-19, barani Afrika imeongezeka ndani ya wiki tano mfululizo zikiwemo nchi jirani na Tanzania.

“Maambukizi yanaongezeka maradufu kuliko ilivyokuwa wimbi la pili,” aliambia wanahabari.

Katika maelezo yake aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono – yaani sanitaiza – na pia kujiepusha na mikusanyiko.

You can share this post!

Kemri kubaini athari ya chanjo kwa Wakenya

Covid: Uganda kuanza kuunda chanjo yake – Rais...