Serikali yaonywa dhidi ya kuhujumu mahakama

Serikali yaonywa dhidi ya kuhujumu mahakama

Na GEORGE ODIWUOR

KAMATI ya Kuangazia Utekelezaji wa Katiba Nchini na Mahakama Kuu zimeonya kuwa huenda Kenya ikajipata pabaya ikiwa serikali itakosa kudumisha uhuru wa Idara ya Mahakama.

Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Peter Kaluma na Jaji wa Mahakama Kuu Aggrey Muchelule waliikosoa serikali kwa kukosa kutambua kwamba Idara hiyo ni taasisi huru ambayo amri zake zinapaswa kutekelezwa.

Viongozi hao hasa walilaumu tawi la utawala la serikali ambalo walilishutumu dhidi ya kuingilia uhuru wa Idara ya Mahakama hivyo kuwanyima Wakenya wengi haki.

Akizungumza Jumanne jioni kwenye ibada ya mazishi katika kijiji cha Ndiru, Eneo Bunge la Homa Bay Town, Bw Kaluma alisema Bunge linaendelea kupokea malalamishi mengi kutoka kwa Wakenya wakilalamika kwamba serikali inakiuka haki zao.

Mawasilisho mengi kwa wabunge huibuka baada ya serikali kukosa kutekeleza amri zinazosubiriwa na walalamishi.

Baadhi ya walalamishi ni Wakenya wanaopaswa kupokea fidia baada ya haki zao kukiukwa.Bw Kaluma alimwagiza Jenerali Kihara Kariuki kuhakikisha kwamba amri za korti zinatekelezwa la sivyo taifa litatumbukia katika sintofahamu.

“Hakupaswi kuwa na mvutano kati ya Idara ya Mahakama na tawi lingine lolote la serikali ili amri za korti zitekelezwe.Hali ya serikali kukosa kutekeleza amri za mahakama inawanyima haki Wakenya kwa kiasi kikubwa jambo ambalo ni hatari kwa sababu kuna uwezekano wa raia kutumbukiza taifa katika michafuko,” alisema.

Hisia zake zilisisitizwa na Jaji Muchelule aliyeongeza kwamba Idara ya Mahakama haitatazama tu huku uhuru wake ukivurugwa.Alitoa wito kwa Wakenya wakiwemo maafisa wa serikali kutii sheria za nchi.

“Taifa linatawaliwa na sheria na uhuru wa Idara ya Mahakama ambao hauwezi kujadiliwa. Itawasadia nyinyi na watoto wenu kutii sheria za mahakama,” alisema jaji.

Idara ya Mahakama imekuwa ikitofautiana na serikali huku Jaji Mkuu anayeondoka David Maraga akizua malalamishi tele kwamba serikali inaingilia kazi.

Miongoni mwa malalamishi hayo ni kukosa kuipa Idara hiyo pesa kwa wakati ufaao na kukosa kuwateua majaji wapya.Idara ya Mahakama pia imekuwa ikikatiwa pesa kwenye bajeti huku fedha zinazodhamiriwa kuendesha shughuli za mahakama zikichelewa kutolewa. Hii imeathiri utekelezaji wa miradi kadhaa ya maendeleo katika idara hiyo.

Bw Kaluma alisema uhuru wa mahakama unapaswa kutekelezwa kupitia utowaji wa fedha kwa wakati ufaao

.“Serikali inapaswa kuipatia fedha Idara ya Mahakama kama njia ya kutekeleza uhuru wa idara hii. Ni makosa kwa serikali kushikilia fedha zilizotengwa Idara ya Mahakama kwenye bajeti na kuwafanya majaji kuonekana kama ombaomba,” alisema muundasheria huyo.

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Teknolojia itatusaidia pakubwa mwaka wa 2021

2020: Waliong’aa na kugusa Wakenya kwa njia ya kipekee