Serikali yapandisha bei ya mafuta baada ya majaji kurarua BBI

Serikali yapandisha bei ya mafuta baada ya majaji kurarua BBI

Na WINNIE ONYANDO

SIKU moja tu baada ya mchakato wa BBI kusambaratishwa na Mahakama Kuu, bei ya bidhaa huenda ikaongezeka kufuatia hatua ya serikali kuongeza bei ya mafuta ya petroli.Mamlaka ya Kawi na Petroli nchini (EPRA) jana iliongeza bei ya mafuta kwa Sh3.56.

Kufuatia taarifa kwa wanahabari, mamlaka hiyo ya Kawi na Petroli katika tangazo lake la kila mwezi kuhusu udhibiti wa bei ya mafuta, ilisema kuwa bei ya petroli itakuwa Sh126.37 kila lita ikilinganishwa na miezi miwili iliyopita ambapo petroli ilikuwa ikiuzwa kwa Sh123 kwa lita.Bei ya mafuta ya taa na dizeli itasalia Sh107.60 na Sh97.85 mtawalia.

Wakazi wa Mombasa watanunua mafuta ya petroli kwa Sh123, dizeli Sh105 na mafuta taa Sh95 mtawalia.Mjini Nakuru, petroli itanunuliwa kwa Sh125.98 huku dizeli ikinunuliwa kwa 107.55 nayo mafuta taa yakiwa Sh97.76.

Petroli itauzwa Sh126.90 jijini Kisumu nayo dizeli na mafuta-taa yatauzwa kwa Sh108.46 na Sh98.68 mtawalia.Wakazi wa Eldoret watanunua mafuta ya petroli kwa Sh126.90 huku dizeli na mafuta-taa yakiuzwa kwa Sh108.46 na Sh98.68.

Kaunti ya mpakani ya Busia petroli itauzwa kwa Sh127.76, dizeli Sh109.33 nayo mafuta ya taa yatanunuliwa kwa Sh99.54.Mamlaka ya EPRA hutathmini bei ya mafuta nchini tarehe 14 ya kila mwezi.

Mwezi uliopita, EPRA haikuongeza bei ya mafuta baada ya Wakenya kutumia mitandao ya kijamii kupinga jaribio la kutaka kuongeza bei.

Kuongezwa kwa bei ya mafuta huenda kukasababisha magari ya umma kuongeza nauli na bidhaa muhimu zinazotegemea mafuta kupanda bei. EPRA jana ilisema kuwa ililazimika kuongeza bei kufuatia ongezeko la bei ya uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka ughaibuni.

EPRA ilisema maamuzi ya bei za mafuta hutolewa kulingana na Idara ya Kawi nchini.Bei hizo mpya zinatarajiwa kutumika kuanzia leo yaani Mei 15 hadi Juni 14.

You can share this post!

ODM wadai Matiang’i anatumia polisi kuwahangaisha Kisii

Jumbe za msamaha, hisani zatawala Idd