NA GEORGE MUNENE
SERIKALI inapanga kufanya mageuzi katika Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) kuhakikisha Wakenya wengi wanamudu gharama ya matibabu ya kansa na magonjwa mengine.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha, ada mpya za NHIF zitatangazwa hivi karibuni.
“Ada ya kila mwezi huenda ikapungua hadi Sh160 kila mwezi. Ni vyema iwapo ada hiyo itapunguzwa ili Wakenya ambao hawajimudu kifedha, nao pia wanufaike,” akasema akihutubia maelfu ya raia katika uwanja wa Runyenjes, Kaunti ya Embu alipozindua rasmi Hamasisho la Kitaifa dhidi ya Saratani mwezi huu Januari.
Alikuwa akimjibu Gavana wa Embu Cecily Mbarire ambaye alipendekeza kuwa ada za NHIF zipunguzwe kutoka Sh500 hadi Sh300.
Bi Mbarire alikuwa amesema kuwa Wakenya wengi hawawezi kumudu kulipa ada ya sasa na akamtaka Bi Nakhumicha kuingilia kati ili pesa hizo zipunguzwe.
“Wakati wa kampeni Rais Ruto alisema kuwa ada za NHIF zingepunguzwa ili kuwanufaisha Wakenya. Tunafanya juu chini kuhakikisha kuwa ahadi ya Rais inatimizwa,” akisema akirejelea ahadi ya Rais kuwa ada hiyo ingepunguzwa kutoka Sh500 hadi Sh300.
Waziri huyo pia alisema kuwa ugonjwa wa saratani ni tishio kubwa nchini kwa kuwa kuna visa vipya 42,000 vinavyotokea kila mwaka pamoja na vifo 27,000.
Subscribe our newsletter to stay updated