Habari za Kitaifa

Serikali yapewa mtihani mkubwa kuhusu Mackenzie

January 9th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

MAHAKAMA ya Shanzu imetishia kumwachilia mhubiri Paul Mackenzie, kiongozi wa dhehebu tata la Good News International, pamoja na washirika wake 29 kwa dhamana ikiwa serikali itakosa kuwasilisha mashtaka dhidi yao ndani ya wiki mbili kuhusu mauaji ya Shakahola.

Hakimu Mwandamizi Mkuu Yusuf Shikanda alisema washukiwa hao wamezuiliwa kwa siku kadhaa kabla kufunguliwa mashtaka hivyo basi safari hiyo lazima ifikie mwisho.

“Iwapo hakuna uamuzi utakaofanywa ya kuwafungulia wahojiwa mashtaka baada ya kumalizika kwa muda huo (siku 14), mahakama itawaachilia watu hao kutoka rumande kwa masharti yatakayoamuliwa na mahakama,” alisema Bw Shikanda

Hakimu alibaini kuwa serikali imekuwa na muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi wa watu hao hivyo kuongeza muda wa siku 180 huku wakisubiri kushtakiwa si halali.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, imeiruhusu serikali siku 14 pekee kuipa muda wa kuamua iwapo itawafungulia watu hao mashtaka yoyote kuhusu tukio hilo ambalo lilishababisha vifo vya zaidi ya watu 429 katika msitu huo wa Shakahola.

Mackenzie na washirika wake 29 wamekuwa kizuizini kwa muda wa siku 117 tangu serikali ilipowasilisha ombi la kuongezewa muda wa kuwazuia kwa siku 180 zaidi.

Hakimu alibaini kuwa maombi ya kuwaweka kizuizini washukiwa hao kwa siku nyingine 180 ilipitwa na wakati kwani muda wa siku 117 imepita tangu ombi hilo liwasilishwa mnamo Septemba 2023.

“Washukiwa wamekaa rumande kwa zaidi ya miezi mitatu tangu ombi la kuongezwa kwa muda wa kuendelea kuwazuilia kuwasilishwa. Imekuwa safari ndefu ambayo lazima ifike mwisho angalau kwa awamu hii,” alisema Hakimu.

Siku 14 zimetolewa kwani ingehitaji muda na vifaa kushughulikia mashtaka kabla ya washukiwa hao kufikishwa mahakamani kutokana na idadi yao.

“Hii ni kutokana na idadi ya washukiwa na mashtaka ambayo wanaweza kukabiliwa nayo. Shughuli hii inaweza tu kufanywa ipasavyo wakati washukiwa watakuwa katika rumande,” hakimu alisema.

Washukiwa hao wamekuwa katika rumande tangu Mei 2023 wakati walikamatwa kuhusiana na maafa katika msitu huo.

Hata hivyo, Mackenzie tayari amepatikana na hatia katika kesi nyingine ambayo alikuwa anakabiliwa na shtaka la kusambaza filamu kinyume na sheria.

Amehukumiwa kwa miezi 18 gerezani.

Kesi hiyo itatajwa tena Januari 23, 2024.