Habari

Serikali yapewa red card

November 19th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta imeshindwa kutekeleza ahadi nyingi zilizotolewa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2017, utafiti umeonyesha.

Utafiti huo uliofanywa na shirika la Mzalendo Trust, umebainisha kuwa, Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto walibuni ujumbe wa kampeni ulionuia kuwashawishi wananchi kwamba watarekebisha makosa yaliyoshuhudiwa katika awamu yao ya kwanza ya uongozi iliyoanza 2013.

Hata hivyo, ikiwa imesalia miaka miwili pekee kabla ya Rais Kenyatta kustaafu kikatiba, ripoti hiyo iliyotolewa jana inaonyesha kuwa ahadi nyingi zilizokuwa katika manifesto ya Jubilee hazijatekelezwa. Dkt Ruto analenga kuwania urais ifikapo mwaka wa 2022.

Kulingana na ripoti hiyo, masuala yanayohusu vita dhidi ya ufisadi, kulinda ugatuzi na usawa wa wananchi kitaifa yamepuuzwa pakubwa.

“Chama cha Jubilee kiliwania uchaguzi mnamo 2017 kikiwa na rekodi mbaya ya uongozi bora, kwani kulikuwa na visa vingi vya ufisadi serikalini, ukosefu wa uwajibikaji, ukiukaji wa haki za binadamu, ubadhirifu na mengineyo. Upande wa upinzani ulikuwa ukishambulia serikali mara kwa mara ukishinikiza kuwepo kwa mageuzi ndipo Jubilee ikabuni ujumbe wa kampeni ukieleza nia ya serikali kubadili mwenendo,” ikasema ripoti hiyo.

Mbali na kushinda urais, Jubilee ilifanikiwa pia kupata viti vingi katika bunge la kitaifa na seneti. Kwa msingi huu, miswada tele imepelekwa bungeni kwa minajili ya kusaidia serikali kufanikisha ahadi zake kwa wananchi, lakini mashinani hali haijabadilika.

“Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wabunge, Jubilee ilitatizika sana kutekeleza ahadi zake nyingi zilizo kwenye manifesto ya 2017, iwe ni kimaendeleo au kuilinda katiba kwa kudumisha usawa, uongozi bora na ugatuzi,” ikasema ripoti ya Mzalendo.

Hali hii inaaminika kuchangiwa na masuala mbalimbali kama vile viongozi walio na malengo ya kibinafsi.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, hatua nyingi zinazochukuliwa serikalini ni kwa msingi ya matakwa ya maafisa wakuu katika Afisi ya Rais badala ya kurejelea ahadi zilizotolewa kwa umma.

Wakati Rais Kenyatta alipotangaza baraza lake la mawaziri, alimtaja Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju kuwa waziri asiyeshikilia wizara yoyote ili kazi yake iwe kuoanisha mipango ya serikali na maazimio ya chama.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa, hili halijasaidia serikali kutekeleza ahadi zake kikamilifu huku muda ukiyoyoma.

Rais Kenyatta alikuwa amezindua Ajenda Nne Kuu, ambazo zilinuiwa kutoa mwelekeo kwa serikali kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kabla aondoke mamlakani mwaka wa 2022.

Lakini wiki iliyopita, Rais aliugeuka msimamo huo akisema Ajenda Nne zinalenga kuacha msingi thabiti wa kimaendeleo wakati atakapokamilisha hatamu yake ya uongozi.

Ajenda hizo zinahusu malengo ya kustawisha viwanda, ujenzi wa nyumba bora za bei nafuu kwa umma, utoaji huduma bora za afya kwa bei nafuu, na uzalishaji bora wa chakula cha kutosha.

Katika mahojiano na wananchi, shirika la Mzalendo Trust lilibainisha kuwa, idadi kubwa ya wananchi inahisi serikali haijatatua suala la usawa kwa kuwa kuna makabila machache yanayoshikilia nyadhifa nyingi serikalini, ikilinganishwa na makabila mengine.

Ilibainika pia kuwa, wanawake, vijana na walemavu wangali wanabaguliwa katika masuala ya kiserikali.

“Karibu ahadi zote zilizotolewa kwa vijana kuwa watahusishwa katika masuala ya kiserikali, hazikutimizwa isipokuwa chache. Ahadi kuhusu usawa wa kijamii hazijatekelezwa,” ikasema ripoti.

Shirika hilo lilipendekeza vyama vya kisiasa viwe vikiunda manifesto ambazo zinaweza kueleweka na umma kwa urahisi na zinazotekelezeka.