Serikali yapewa siku 7 kuzuia mgomo wa wahadhiri

Serikali yapewa siku 7 kuzuia mgomo wa wahadhiri

Na FAITH NYAMAI

SHUGHULI za masomo katika vyuo vikuu vya umma huenda zikatatizika baada ya wahadhiri kutishia kugoma wiki ijayo iwapo serikali haitawalipa nyongeza ya mishahara.

Katibu Mkuu wa Chama cha Waadhiri wa Vyuo vya Umma (Uasu), Constantine Wasonga jana alitoa makataa ya siku saba kwa serikali kuwalipa nyongeza ya mishahara kwa mujibu wa Mkataba wa Maelewano (CBA) wa 2017-2021.

Dkt Wasonga alisema wahadhiri wa yuo vikuu hawatakubali visingizio ambavyo vimekuwa vikitolewa na wakuu wa vyuo vikuu huku akitaka fedha zao kutolewa mara moja.

“Tunatoa ilani ya siku saba kabla ya kugoma. Hii ni kwa sababu Jukwaa la Ushauri la Baraza la Vyuo Vikuu vya Umma (IPUCCF) na serikali limekiuka maagizo ya korti ya kuwalipa wafanyakazi wa vyuo,” akasema Dkt Wasonga.

Wanaotarajiwa kujiunga na mgomo huo ni pamoja na maprofesa, maprofesa washirika, wahadhiri wakuu, wahadhiri, wahadhiri wasaidizi na wakufunzi waliohitimu.

Wanashutumu vyuo vikuu kwa kuzuia sehemu ya mishahara yao na kuwalipa chini ya mishahara iliyojadiliwa. Korti ya Uhusiano wa Ajira na Kazi mnamo Januari 15, 2021 iliamuru CBA itekelezwe kikamilifu kwa kufuata sheria ya kuwalipa wafanyikazi wa vyuo mishahara, jambo wanalosema halijatekelezwa.

Katika uamuzi wa korti, gharama ya CBA ilitolewa kuwa Sh13.812 bilioni bila kujumuisha pesa ya kustaafu. Hapo awali, Tume ya Mishahara ilisema kuwa jumla ya gharama ya CBA ni Sh8.8 bilioni.Hata hivyo, Dkt Wasonga alisema hadi sasa IPUCCF haijatekeleza amri ya korti.

“Leo tunatoa ilani ya mapema ya mgomo wa siku saba na tunatarajia wafanyakazi wote wa vyuo vya umma watuunge mikono,” akaongezea Dkt Wasonga.

Kwa upande wao, wajumbe wa kamati kuu ya kitaifa walliohudhuria mkutano huo waliunga mkono kanuni hiyo ya Uasu wakisema kuwa wote wamekubaliana na mgomo huo wa kutaka mishahara kutolewa.Dk Wasonga alionya kuwa wafanyikazi wa vyuo vya umma hawataendelea kuwa watumwa tena.

Alikiri kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu Chansela Geoffrey Muluvi aliwaambia wiki moja iliyopita kuwa vyuo vikuu havina fedha za kuwalipa wafanyikazi mishahara.

“Ikiwa hawana pesa, basi wajiuzulu kutoka nafasi hizo mara moja, si jukumu la Uasu kutafuta pesa za kuheshimu usimamizi na majukumu ya serikali, jukumu letu ni kujadili CBA,” akasema Dk Wasonga.

Kadhalika, alisema kuwa hata Sh8.8 bilioni ambazo SRC na IPUCCF zilitoa hazijatolewa kwa wahadhiri.Mwenyekiti wa Uasu, Grace Nyongesa alisema tawala za vyuo vikuu zimepuuza kwa makusudi amri ya korti inayowaamuru walipe mishahara kamili.

“Hatutalala hapa, tutaendelea kupigania haki za wafanyikazi wa vyuo katika nchi hii, sisi ndio tunaowafundisha wahandisi katika nchi hii. Hatuwezi kuendelea kudharauliwa na kutishiwa mara kwa mara,” akasema Dkt Nyongesa.

Kulingana na Uasu, vyuo vikuu saba tu kati ya 35 ndivyo vimewalipa wahadhiri wao kulingana na ripoti yao sahihi.

Dkt Nyongesa alisema kuwa vyuo vikuu kama vile Chuo Kikuu cha Nairobi, Chuo Kikuu cha Kenyatta, Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya wanawalipa wahadhiri wao mshahara duni.

You can share this post!

Watu 18,000 waokolewa kwa meno ya Taliban

Vigogo wa kisiasa kutafuta mbinu mpya kusuka miungano bila...