Habari za Kitaifa

Serikali yaruhusu mchakato wa kusaka mabaki ya shujaa Dedan Kimathi

February 18th, 2024 1 min read

NA JAMES MURIMI

SERIKALI imeruhusu kuanzishwa rasmi kwa mchakato wa kutafuta mabaki ya aliyekuwa shujaa wa wapiganaji wa Mau Mau, marehemu Dedan Kimathi, miaka 67 baada ya kifo chake.

Hali hiyo imewaletea matumaini katika familia ya marehemu Field Marshal Dedan Kimathi baada ya muungano wa wataalamu kutoka Kenya na kote duniani kuungana kuchapa kazi hiyo.

Aidha, familia hiyo inathamini sana sanamu ambayo iliwekwa kwa heshima ya mpiganiaji uhuru wa Kenya nyumbani kwake katika Kijiji cha Karuna-ini, Kaunti ndogo ya Tetu, Kaunti ya Nyeri.

Mnamo 1957, mwili wa Kimathi, kiongozi shupavu na jasiri katika vita vya Maumau, ulitolewa nje ya chumba alichotiwa kitanzi ukiwa na kamba shingoni mwake.

Alipokuwa anazikwa katika kaburi lisilojulikana, serikali ya Uingereza na walowezi waliingia barabarani kusherehekea kifo cha ‘gaidi’ na amani ambayo ingefuata.

Kwao, kifo chake kilimaanisha mwisho wa vita ambavyo vilikusudiwa kuchochea uhuru wa Kenya.

Mnamo Februari 29, 2024, Rais William Ruto anatarajiwa kuzindua rasmi msako wa mabaki ya Kimathi, ambapo wataalamu wataanza shughuli hiyo.