Serikali yaruhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje

Serikali yaruhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI imeruhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje bila kulipiwa ushuru kama hatua ya kupunguza uhaba wa zao hilo nchini na makali ya baa la njaa linalowakeketa jumla ya Wakenya 3.5 milioni nchini.

Kulingana na tangazo lililochapisha na Waziri wa Fedha Ukur Yatani kwenye gazeti rasmi la serikali Mei 20, 2022 ni jumla ya tani 540,000 zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini kabla ya Agosti 6, 2022.

“Kulingana na sheria husika na ilani iliyotolewa na Waziri wa Kilimo kuhusu uhaba wa mahindi nchini, nimeagiza kuondolewa kwa ushuru wa uagizaji wa mahindi yaliyozidi tani 540,000 kutoka nje. Mahindi hayo yasiwe yale ambayo yamezalishwa kisayansi (GMO),” Bw Yatani akasema katika notisi hiyo.

Mahindi hayo yanaweza kuagizwa nje ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika notisi hiyo, serikali inashikilia kuwa ni mahindi meupe pekee yataagizwa kutoka nje na shehena zote sharti zizingatie masharti yaliyowekwa.

Masharti hayo ni kama yafuatayo;

a) Mahindi yatakayoagizwa kutoka nje yasiwe yale ambayo yamezalishwa kisayansi (GMO) kulingana na sheria za Kenya na viwango vilivyowekwa na Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa (KEBs) na Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Mazao yaliyozalishwa Kisayansi (NBA).

b) Mahindi yatakayoagizwa sharti yawe na kiwango cha unyevunyevu kilichozidi asilimia 13.5 inayokubalika kulingana na sheria za Kenya.

c) Kiwango cha sumu ya aflatoxin katika kila shehena hakifai kuzidi 10 ppb inavyohitajika chini ya sheria za Kenya na viwango vilivyowekwa na KEBS na Wizara ya Afya.

d) Mahindi yaliyoagizwa kutoka nje sharti yaandamanishwe na cheti cha kibali kilichotolewa na Kebs.

e) Mahindi hayo yameagizwa ndani ya miezi mitatu kati ya sasa na Agosti 6, 2022.

f) Mahindi hayo sharti yatimize mahitaji yote ya kisheria chini ya sheria za Kenya.

Uhaba wa mahindi nchini umeathiri shughuli za kampuni za kusaga unga na hivyo kuchangia kuongezeka kwa bei ya unga wa mahindi madukani nchini.

Bei hiyo imepanda kutoka Sh100 kwa paketi moja ya kilo mbili Januari 2022 hadi Sh160 wakati huu katika maduka jijini Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Wanaraga wa Kenya Simbas wang’atwa na Boland ligi ya...

Wadau wataka serikali ifufue mpango wa chakula kwa wanafunzi

T L