Serikali yasema haijui walikoenda watahiniwa 12,000 wa KCPE

Serikali yasema haijui walikoenda watahiniwa 12,000 wa KCPE

Na FAITH NYAMAI

SERIKALI imeshindwa kueleza walikoenda wanafunzi 12,424 waliojisajili kufanya mtihani wa KCPE 2020, shule zilipofunguliwa tena kufuatia likizo ndefu iliyosababishwa na janga la Covid-19.

Licha ya kuwashirikisha machifu na manaibu chifu kuhakikisha wanafunzi wote walirejelea masomo yao shule zilipofunguliwa mnamo Oktoba mwaka uliopita na Januari mwaka huu, Wizara ya Elimu imeshindwa kueleza walipo maelfu ya watahiniwa na wanafunzi wengine ambao hawakurejea shuleni.

Huku wanafunzi kadhaa wakiripotiwa kufariki kabla ya kuanza mitihani yao, wengi wao, karibu asilimia 80, waliripotiwa kukataa kurudi shule huku wengine wakihama walipokuwa wakiishi ambapo walimu wakuu hawangeweza kuwapata.

Kutokana na likizo ndefu nyumbani, idadi ya mimba za mapema iliongezeka huku wengine wakiripotiwa kujihusisha katika mihadarati na shughuli nyinginezo za uhalifu.

Ingawa Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alitaja idadi ya waliokosa kufanya mitihani hiyo kama “isiyotishia” ikilinganishwa na jumla ya wanafunzi 1,179,192 walioshiriki mitihani hiyo, idadi hiyo iliongezeka maradufu ukilinganisha na waliokosa kufanya mitihani hiyo mwaka uliopita.

Mnamo 2019, ni jumla ya wanafunzi 5,530 pekee waliokosa mitihani hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumza na Taifa Jumapili jana, Katibu wa Wizara ya Elimu, Julius Jwan, alisema idadi kubwa ya watahiniwa waliokosa mitihani hiyo ni kutoka jamii za wafugaji na wasichana chipukizi ambao ama walipachikwa mimba au walioozwa wangali wachanga ambao walikataa kurejea shuleni.

Dkt Jwan alisema baadhi ya wavulana walijiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na wengine kugeukia biashara ya bodaboda. Baadhi yao walijiingiza katika vibarua vidogovidogo ili kutafutia riziki familia zao.

“Kwa mfano, nilipoongoza kikosi katika Kaunti ya Tana River kuwakusanya wanafunzi warejee shuleni, tuligundua baadhi yao walikuwa wamehama katika maeneo mengine na walimu hawangeweza kuwasiliana na wazazi wao kwa simu kwa sababu hawana nambari zao,” alifafanua.

Dkt Jwan alisema kuwa licha ya likizo ya miezi saba kutokana na janga la Covid-19, Wizara za Elimu na Usalama wa Nchi zilishirikiana pamoja kupitia machifu na manaibu chifu na kuhakikisha idadi kubwa ya watahiniwa walirudi shuleni.

“Katika kiwango cha Wizara, tunafuatilia kubaini ni wapi watahiniwa hawa walipo na kuhakikisha wanarejea shule,” alisema

You can share this post!

Kipchoge asahau masaibu ya London Marathon kwa kubeba taji...

ODM yakana Oparanya aelekea kwa Ruto