Habari

Serikali yasema haitarajii drama kurejea kwa Miguna Miguna

January 6th, 2020 2 min read

Na MARY WAMBUI

SERIKALI imekariri kwamba hakutarajiwa drama na mvutano wowote wakili Miguna Miguna akitarajiwa kutua nchini Kenya akitokea nchini Canada.

Aidha, Idara ya Uhamiaji imesema itafanikisha kurejea nchini kwake ikiwa sehemu ya kutii maagizo yaliyotolewa na mahakama mwaka 2018.

Machi 2019 wakili huyu alilazimishwa kusafiri hadi nchini Canada ambako ana uraia pia.

Dkt Miguna ambaye tayari ameabiri ndege ya shirika la Lufhthansa kuelekea jijini Nairobi ametangaza atatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Jumanne saa 9.25 usiku baada ya kukaa Canada karibu kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumza na ‘Taifa Leo’, Msemaji wa Serikali Kanali Cyrun Oguna amesema Jumatatu kwamba kauli ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu kurejea kwa Dkt Miguna inazingatiwa kikamilifu.

Amesema wakili huyo ataruhusiwa nchini kama tu raia yeyote mwingine.

“Kiongozi wa nchi alitangaza kwamba (Miguna) yuko huru kurudi na huo ungali msimamo wa serikali,” amesema Kanali Oguna.

Rais Uhuru Kenyatta kwenye mazishi ya mpiganiaji uhuru wa pili Charles Rubia katika Kaunti ya Muran’a, alisema kila raia ana uhuru wa kutoa kauli zake na vilevile akasema Miguna yuko huru kurejea nchini.

“Nimesikia kuna wale wanapanga kusafiri kuja humu nchini; nawaambia wako huru kufanya hivyo,” akasema kiongozi wa nchi.

 

Ingawa hivyo, Kanali Oguna amesema anatarajia Miguna kutii kanuni na utaratibu wote muhimu kwa wasafiri kumaanisha kwamba asijichukulie kuwa ni mtu spesheli anayehitaji angalizo maalum.

“Ni sharti awe na stakabadhi muhimu zinazohitajika,” amesema Oguna.

Jumatatu mchana Mkurugenzi wa Uhamiaji Alexander Muteshi amesema watahakikisha watafanikisha kurejea kwa Miguna.

“Idara imefahamishwa kwamba Dkt Miguna Miguna atasafiri kuingia nchini Kenya mnamo Jumanne, Januari 7, 2020,” amesema Muteshi katika taarifa.

Akaongeza: “Hii ni sehemu mojawapo ya kutii maagizo yaliyotolewa na mahakama Desemba 14, 2018.”

Miguna alipokuwa nchini Kenya mara ya mwisho alionekana machoni pa serikali ya Jubilee kama kitisho kwa usalama wa nchi.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, Miguna amesema Jumatatu asubuhi kwamba hatarajii kuchukuliwa kama mtu spesheli.

“Ninapigania haki zangu na ninataka ziheshimiwe. Ninataka paspoti yangu ya Kenya tena ikiwa katika hali nzuri. Ninataka maagizo yaliyotolewa na mahakama yakiheshimiwa. Ninafaa kuingia nchini Kenya bila vikwazo kwa sababu mimi ni raia halisi,” ameandika Miguna.

Ombi la wakili huyo lilikubalika ambapo mahakama iliagiza arejee nchini kupitia utambulisho wa kitambulisho cha kitaifa au paspoti yake inayoshikiliwa na serikali.