Serikali yasema itaondoa barabarani matatu zionazokaidi kanuni  za corona

Serikali yasema itaondoa barabarani matatu zionazokaidi kanuni za corona

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imeonya kwamba itaadhibu matatu zinazokiuka sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia msambao wa virusi vya corona katika sekta ya usafiri na uchukuzi.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alisema Jumatano kwamba zitaondolewa barabarani kwa kulemaza vita dhidi ya corona.

Bw Kagwe pia alisema leseni za miungano inayomiliki matatu hizo huenda zikafutiliwa mbali.

“Matatu ambazo zinaendelea kukiuka kanuni na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia kuenea kwa Covid-19 zitachukuliwa hatua. Isitoshe, leseni za miungano inayozimiliki itafutiliwa mbali,” akaonya Waziri Kagwe.

Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa Homa ya virusi vya corona, serikali iliamuru magari ya uchukuzi wa umma kubeba asilimia 60 ya idadi jumla ya abiria, wanaosafirishwa mara moja.

Vilevile, kila gari la usafiri na uchukuzi linapaswa kutakasa abiria mikono kabla ya kuwaruhusu kuingia na pia kuhakikisha wamevalia barakoa.

“Ninakumbusha wahudumu wa matatu, hakuna abiria anayepaswa kubebwa bila maski,” akasisitiza Bw Kagwe.

Mapema Jumatano, kamatakamata ya matatu zinazokiuka sheria na mikakati zilizopendekezwa na Wizara ya Afya ilishuhudiwa katika Kaunti ya Nakuru.

Katika siku za hivi karibuni, idadi ya visa vya maambukizi ya corona inayoandikishwa kila siku imeonekana kuongezeka.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Handisheki itakufa baada ya refarenda

Rais wa Tanzania John Magufuli afariki