Habari Mseto

Serikali yasema SGR ilipata Sh5.7b, Uchina yasema ni Sh10.3b. Nani msema kweli?

May 28th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Huenda reli ya kisasa kati ya Nairobi na Mombasa ilipata hasara, miaka miwili baada ya kuzinduliwa nchini.

Serikali imedurusu mapato kutokana na SGR katika mwaka wa kwanza (Juni 2017- Juni 2018)  ambayo yamepungua kwa asilimia 44.

Hatua hiyo imeibua maswali kuhusiana na ikiwa habari zinazotolewa kuhusu operesheni za mfumo huo ni za kweli.

Habari rasmi zilizotolewa Ijumaa na serilali zinaonyesha kuwa SGR ilipata Sh5.7 bilioni mwaka 2018, hasa kutokana na uchukuzi wa mizigo.

Takwimu hizo ni tofauti na takwimu zilizotolewa Machi zilizoonyesha SGR ilipata Sh10.33 bilioni, kulingana na balozi wa China nchini Wu Peng.

Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu (KNBS) ilikataa kutoa sababu za kushusha kiwango cha mapato kwa asilimia hadi 44, na kuzua maswali kuhusiana na data inayokusanywa kuhusu SGR.

Inamaanisha kuwa huenda mradi huo ukachukua muda kabla ya kuanza kupata faida.

Kulingana na data ya awali, mapato ya SGR yalikuwa ni Sh10.33 bilioni dhidi ya gharama ya operesheni ambayo ilikuwa ni takriban Sh12 bilioni.

Shughuli ya uchukuzi wa mizigo ilianza Januari 2018 na iliipa SGR Sh4 bilioni kufikia Desemba dhidi ya tangazo la awali la Sh8.72 bilioni kulingana na takwimu hizo za KNBS.

Kulingana na takwimu hizo kampuni ya CCCC, ambayo huendesha SGR, iliuza tiketi 1.66 milioni na kupata Sh1.61 bilioni wakati huo.