Habari

Serikali yasema waliofurushwa Kariobangi walihadaiwa kununua vipande vya ardhi

May 6th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SIKU kadhaa baada ya baadhi ya wakazi Kariobangi, Nairobi, kuachwa bila makao kufuatia ubomoaji wa nyumba zao, serikali imejitokeza na kueleza kwamba walihadaiwa kununua ardhi.

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i  amesema Jumatano waathiriwa wanahangaika kwa sababu ya matapeli wa vipande vya ardhi.

“Wengi wao hawana hatia, walitapeliwa kununua vipande vya ardhi ambavyo ni mali ya umma,” Dkt Matiang’i amesema.

Ubomoaji huo wa mnamo Jumatatu, uliwaacha wengi kukesha kwenye kijibaridi kikali, wakati huu ambapo taifa na ulimwengu umekodolewa macho na janga la Covid-19.

Kulingana na waziri Matiang’i ni kwamba ardhi hiyo inamilikiwa na kampuni ya usambazaji maji ya Nairobi Water & Sewerage Company.

“Ardhi hiyo ni ya umma, imetengewa kampuni ya Nairobi Water kuimarisha utendakazi wake,” waziri akasema, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kufuatilia na kutwaa ardhi za umma zilizonyakuliwa.

Kuangazia masaibu yanayofika waathiriwa, Dkt Matiang’i amesema atajadiliana na Shirika la Huduma za jiji la Nairobi (NMS) ili kuwasaidia.

Ubomoaji wa Kariobangi ulijiri wiki kadhaa baada ya serikali kufanya ubomoaji mwingine eneo la Ruai, Nairobi, katika ardhi inayodaiwa kunyakuliwa na matapeli.