Habari Mseto

Serikali yashauri familia zihakikishe maiti za wanaozirai na kufariki ghafla zinapimwa

August 2nd, 2020 2 min read

VALENTINE OBARA na BENSON MATHEKA

SERIKALI imeagiza familia zihakikishe mtu yeyote anayekufa ghafla bila dalili za kuugua, maiti yake inapimwa kuthibitisha kama alikuwa ameambukizwa virusi vya corona au la.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya, Dkt Patrick Amoth alisema Jumamosi inafaa kuthibitisha kiini cha kifo, kwani ni hatari watu kuruhusiwa kuzika wapendwa wao wanaozirai na kufariki ghafla wakati huu wa janga la corona.

Kulingana na Dkt Amoth, imethibitishwa baadhi ya watu wanaofariki kwa virusi vya corona hawana dalili zozote za ugonjwa wowote.

“Unaweza kuwa unahisi vyema lakini mapafu yako yameharibiwa na corona,” akaeleza.

Alisema hayo wakati nchi ikiendelea kupata idadi kubwa ya watu wanaofariki kwa ugonjwa huo.

Jumamosi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza kuwa watu 23 walifariki na kufikisha idadi ya jumla hadi 364.

Katika kipindi cha saa 24 kilichokamilika Jumamosi, watu 727 walipatikana wameambukizwa virusi hivyo na kufikisha idadi hadi 21,363.

Hata hivyo, wengine 254 walipona na hivyo idadi ikafika 8,419.

Hatua iliyotangazwa na Dkt Amoth ilitokana na visa vya watu kuzirai na kufariki ghafla katika sehemu mbalimbali za nchi katika wiki kadhaa majuzi.

Kuanzia mwezi uliopita, visa zaidi ya saba vya watu kuzirai ghafla na kufariki vimeripotiwa maeneo tofauti nchini.

Hapo jana, mwanamume alizirai na kufariki katika kituo cha biashara cha Chaka, Kaunti ya Nyeri na mwingine katikati mwa jiji la Nairobi.

Wiki iliyopita, mkuu wa polisi eneo la Bondo (OCPD), Antony Wafula alianguka na kufariki.

Mnamo Julai 20, mwanume alianguka na kufariki baada ya kushuka matatu mtaani Dandora.

Siku chache baada ya kisa hicho kuripotiwa, afisa wa polisi aliyekuwa akilinda benki ya Equity mjini Meru alianguka na kufariki akiwa kazini.

Mnamo Julai 23, 2020, mwanamume alizirai na kuaga dunia nje ya duka moja mtaani Mwihoko, Nairobi.

Katika kisa kingine jijini Nairobi, Kijana wa kurandaranda mitaani alianguka na kufariki ghafla akilalamikia maumivu ya kifua.

Kisa kama hicho kiliripotiwa katika kijiji cha Kitivo, Kaunti ya Makueni, ambapo mzee mmoja alianguka na kufariki baada ya kupata matatizo ya kupumua.

Katika Kaunti ya Kiambu, dereva wa teksi alizirai na kufariki akiwa ndani ya gari lake nje ya hospitali moja mjini Juja.