Habari

Serikali yashauriwa iombe kuongezewa muda wa kulipa mkopo kutoka China

April 24th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI sasa inatakiwa kuomba iongezewe muda wa kulipa deni inalodaiwa na China la kima cha takriban Sh634 bilioni.

Ushauri huo ulitolewa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi kuhusu Masuala ya Kiuchumi (IEA) Kwame Owino ambaye amealezea hofu kwamba huenda uchumi wa Kenya ukaathirika ikiwa serikali italipa deni hilo kwa wakati uliowekwa.

Kulingana  Bw Owino katika mwaka huu wa kifedha serikali inatarajiwa kutumia Sh870 bilioni itakazokusanya kama ushuru kulipia madeni yake, haswa yale ya kigeni.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Masuala ya Kiuchumi, Institute of Economic Affairs (IEA), Kwame Owino. Picha/ Maktaba

“Ikiwa kiwango kama hiki cha pesa kitatumiwa kulipa madeni, huenda serikali ikakosa pesa za kuendesha shughuli zake za ndani kama ufadhili wa miradi. Hii ndiyo maana tunaitaka serikali kuanzisha mazungumzo na China ili iongezewe muda wa kulipa deni hadi mwaka wa 2024 ili uchumi wa nchi usiathirike kwa njia hasi,” Kwame akawaambia wanahabari Jumatano.

Serikali inapaswa kuanza kulipa mkopo wa kima cha Sh497 bilioni ambao ilikopa kutoka China kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ya Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Mombasa hadi Nairobi na awamu ya 2A kutoka Nairobi hadi Naivasha.

Kufaidi Wakenya

IEA inapendekeza kuwa serikali ikope kutoka mashirika ya kifedha ya humu nchini ikisema hatua hiyo itafaidi Wakenya wengi.

Wakati huu, ujumbe wa Kenya ukiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga uko nchini China kujadili ombi la mkopo wa Sh368 bilioni za kufadhili ujenzi wa awamu ya 2B ya SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Bw Owino anapendekeza Kenya ibadili mwenendo wake wa kuchukua mikopo yenye riba ya juu kama vile Eurobond au mkopo kutoka China akisema mikopo hiyo ni ghali kwa mlipa ushuru.

IEA pia inapendekeza kuwa serikali ikope kutoka humu nchini kupitia hati za dhamana ambazo ni zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wawekezaji wa humu nchini.

Kwa ujumla kulingana na taasisi hiyo, kufikia Septemba 2018 kiwango cha deni la serikali kilikuwa ni Sh5.15 trilioni, ikijumuisha Sh2.54 trilioni kama mkopo kutoka humu nchini na  Sh2.16 trilioni kama mkopo wa nje.