Habari

Serikali yasitisha ubomoaji zaidi Kariobangi

May 9th, 2020 1 min read

NYAMBEGA GISESA na CHARLES WASONGA

SERIKALI imesitisha ubomoaji zaidi katika kitongoji duni cha Kariobangi Sewerage kilichoko katika mtaa wa Kariobangi North, Nairobi baada ya wakazi kufanya maandamano wakikosoa kufurushwa huko kutoka kipande cha ardhi cha kutumiwa kwa upanuzi wa eneo la kusafishwa kwa majitaka.

Uamuzi huo ulitangazwa na Mshirikishi wa Kaunti ya Nairobi Wilson Njenga ambaye pia alisema maafisa wa usalama wanajaribu kuleta utulivu katika eneo hilo.

Haya yalifikiwa Ijumaa katika mkutano wa mashauriano ulioongozwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na kuhudhuriwa na mawaziri wenzake, Sicily Kariuki (Maji) na Mutahi Kagwe (Afya).

Mkutano huo ambao uliitishwa kuhakiki mikakati iliyowekwa kuzuia kuenea kwa Covid-19 katika Kaunti ya Nairobi na maeneo ya karibu pia uliamua kuwa soko la Kogorocho liruhusiwe kuendelea na shughuli kama kawaida.

Mnamo Jumatatu, zaidi ya familia 7,000 ambazo zimeishi katika kitongoji cha Kariobangi Sewerage ziliachwa bila makao baada ya nyumba zao kubomolewa na Kampuni ya Maji na Majitaka ya Nairobi (NCWSC) chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Kampuni hiyo inadai kuwa kipande hicho cha ardhi cha ukubwa wa ekari 10 ni mali yake na kwamba kilinyakuliwa na wakazi hao chini ya mwavuli wa muungano wa Kariobangi Sewerage Self Help Group mnamo 2008.

Lakini NCWSC inadai watu hao walinyakua ardhi kutoka kwa kampuni shirikishi ya Dandora Estate Sewerage Treatment Plant iliyoko Ruai.

Kampuni hiyo ilisema inapanga kutumia ardhi hiyo kupanua eneo la kusafisha majitaka; mradi ambao unalenga kugharibu Sh4 bilioni.

Lakini wakazi hao walidai kuwa wao ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo na walipewa na lililokuwa baraza la jiji la Nairobi wakati wa hatamu za uongozi wa meya wa zamani Dick Waweru mnamo 1996.

Wakati wa maandamano Ijumaa wakazi hao walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati mzozo huo ili warejeshewe ardhi ‘yao’.