Habari za Kitaifa

Serikali yasitisha zabuni za mashirika ya umma kukata matumizi

March 28th, 2024 2 min read

NA BRIAN AMBANI

SERIKALI imepiga marufuku zabuni ya ununuzi wa vifaa vyenye nembo za idara mbalimbali za serikali, kama njia ya kupunguza matumizi katika wizara na mashirika ya umma.

Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amewaandikia memo makatibu wa wizara na wakuu wa mashirika ya serikali, akiwaamrisha wapunguze matumizi ya pesa kwa mambo ambayo hayapewi kipaumbele katika utoaji huduma kwa raia.

Bw Koskei aliwaamrisha wakuu hao wasitumie pesa katika kununua kalenda, shajara, miavuli, mikopo, vikombe, vitabu vya kunakili mambo kati ya vifaa vingine.

“Unaamrishwa mara moja usitishe utoaji zabuni, kuchapisha na kutoa mavazi kwa wafanyakazi wa mashirika ikiwemo mashati, mashatitao, jezi na nguo nyingine ambazo zina nembo za kampuni au idara za serikali,” akasema Bw Koskei.

Pia, Bw Koskei alisema kuwa amri hiyo ni sehemu ya mpango wa kiuchumi wa serikali kupunguza matumizi ya wizara na mashirika ya serikali wakati huu taifa linapokuwa pabaya kiuchumi.

“Amri hii inasisitiza kutotumika kwa pesa katika matumizi ambayo hayana umuhimu sana kwa raia. Inalenga kukata matumizi ya serikali na itatekelezwa bila kuhujumu utendakazi wa serikali,” akaongeza.

Matumizi makubwa ya fedha katika serikali yamemfanya Rais William Ruto ajikune kichwa tangu aingie mamlakani mnamo Septemba 2022.

Mwaka huo alitangaza kuwa amekata bajeti kwa Sh300 milioni ili kutoa nafuu kwa Hazina Kuu ya Fedha.

Mnamo Oktoba 2023, Rais Ruto aliamrisha kuwa maafisa wa serikali hawafai kutumia pesa kiholela kwa masuala ambayo hayanufaishi raia au kuboresha utoaji wa huduma kwao.

Kwenye mwongozo mpya uliotolewa, ziara za maafisa wa serikali katika mataifa ya kigeni zinafadhiliwa tu pale ambapo wana wajibu muhimu wa kutekeleza katika mikutano wanayohudhuria.

Amri ya Bw Koskei inajiri wakati ambapo serikali imekaza kamba katika matumizi yake huku mapato yakikosa kufikia kiwango kinacholengwa. Hii inamaanisha kuwa serikali lazima isawazishe matumizi yake na pia kiwango cha hela kinachokusanywa.

Kufikia Februari Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru Nchini (KRA) ilikuwa imekusanya Sh1.374 trilioni ambayo ni asilimia 55 ya Sh2.495 trilioni ambazo zinalengwa na serikali mwaka huu wa kifedha.

KRA sasa ina kibarua cha kukusanya Sh1.121 trilioni kati ya Machi na Juni ambazo ni Sh280.25 bilioni kila mwezi.