Serikali yataka walimu warudishe ‘karo’ haramu

Serikali yataka walimu warudishe ‘karo’ haramu

Na VICTOR RABALLA

WIZARA ya Elimu imeamrisha walimu wakuu warejeshe pesa ambazo wamezipokea kwa njia ya haramu au kuziongeza kama karo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo yao shuleni.

Katibu katika Wizara ya Elimu, Dkt Julius Jwan alisema Jumanne kwamba malalamishi yamekuwa yakipelekwa kwa wizara kuhusu baadhi ya walimu wakuu kupokea pesa kwa njia isiyofaa kutoka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wasiojiweza katika jamii.

“Kuna baadhi ya wanafunzi ambao wamekuwa wakiwekewa mabaki ya karo ya uongo kisha kufukuzwa nyumbani. Usimamizi wa shule umekuwa ukiwadai pesa ambazo tayari zimelipwa ilhali hazionekani katika hesabu za shule,” ikasema taarifa kutoka wizara hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari na Taasisi za Masomo, Paul Kibet.

Aidha, Bw Jwan alisema shule yoyote ambayo ingependa kuongeza karo kuliko kiwango kilichowekwa, inafaa itume barua kwa wizara kupewa idhini.

Ingawa hivyo, aliamrisha kuwa hakuna mwanafunzi anayefaa kufukuzwa shuleni kwa kukosa kulipa karo huku akitaka shule zote kuweka nakala ya karo wanazotoza katika bango la shule.

Iwapo kuna shule ambazo zinatoza pesa za mlo wa chamcha, basi pesa hizo zinafaa zitolewe kwa hiari na si lazima kwa wanafunzi wote kama njia ya kuhakikisha kuna uwazi.

Pia taarifa yote ya kiwango cha karo inayotozwa inafaa kutoka kwa Waziri wa Elimu wala shule hazina uhuru wa kubadilisha kiwango hicho kilichopitishwa na wizara.

Kwenye barua ya Bw Kibet, wasimamizi wa bodi za shule mbalimbali ambao wanapitisha utozaji wa karo haramu watachukuliwa hatua kali ikiwemo kufikishwa kortini.

Wazazi, hasa wale wa shule za upili ambao wanahisi wamedhulumiwa kwa kutakiwa walipe karo zaidi wapige ripoti kuhusu hatua hiyo kupitia baruapepe directorsecondary2018@gmail.com ndipo suala hilo lifuatiliwe na hatua zifaazo kuchukuliwa.

“Kulingana na kanuni zilizopo, wakurugenzi wa elimu kwenye kaunti na kaunti ndogo wametakiwa waripoti kwa Katibu wa Wizara, bodi yoyote ya usimamizi wa shule ambayo inatoza karo haramu mara moja,” ikaongeza.

Kumekuwa na madai kuwa baadhi ya walimu wakuu wamekuwa wakitoza karo ya juu kuliko iliyopitishwa na wizara kwa kila shule husika.

You can share this post!

Vyakula vya kuepuka kama una ngozi ya mafuta

NGILA: Toka mjini, uchumi wa kidijitali umefika vijijini