Habari Mseto

Serikali yatakiwa kutaja wanyakuzi wa msitu wa Mau

July 12th, 2018 2 min read

GEORGE SAYAGIE na PATRICK LANG’AT

SERIKALI inaendelea kukabiliwa na shinikizo za kuwafichua na kuwashtaki mabwenyenye walionyakua ardhi katika Msitu wa Mau na kuwauzia Wakenya ambao sasa wanatimuliwa katika mashamba hayo kwa kukosa vyeti vya umiliki.

Shughuli ya kuzitimua zaidi ya familia 600 tayari imeanza huku wazee wa jamii husika wakiitaka serikali kufichua wafanyabiashara laghai waliowatapeli wakazi.

Baraza la Wazee wa jamii ya Maasai jana lilitaka serikali kutoa hadharani majina ya wahusika kisha iwachukulie hatua za kisheria.

Wengine ambao wanataka mabwenyenye hao wafichuliwe na kushtakiwa ni pamoja na Baraza la Wazee kutoka Rift Valley kupitia mwenyekiti wake Gilbert Kabage na Wazee wa Ogiek kupitia mwenyekiti wake Joseph Towett.

“Wahusika wakuu katika sakata hii wako katika ripoti ya Jopo la Waziri Mkuu (Raila Odinga) iliyowasilishwa bungeni na wanapaswa kutangazwa hadharani. Serikali inawafahamu vyema,”alisema Joseph Ole Karia, ambaye alikuwa mwanachama wa Jopo la Mau Forest.

Bw Karia ambaye pia ni katibu wa Baraza la Wazee wa Maasai alisema wanyakuzi wa mashamba ya msitu huo wamo katika ripoti ya 2008 iliyowasilishwa bungeni mnamo 2009.

Zaidi ya watu 2,000 kutoka familia 333 tayari wametimuliwa kutoka Msitu wa Maasai Mau, ambao ni sehemu ya Msitu mkubwa wa Mau Complex.

Mau Complex unajumuisha maeneo ya Transmara, Ol Posimoru, Eastern Mau, Mau Narok, South West Mau, Western Mau, Mlima Londiani, Eburru, Molo na South Molo.

Baadhi ya watu waliotajwa Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni mnamo 2009 ni pamoja na diwani wa zamani Korema Ole Surum (ekari 2,988), Bw Francis Lemiso Kipturkut (ekari 2,653), Ololarusi Investment Farm (ekari 4,001), na IIngina Contractors (ekari 1,295).

Jana, Kamishna wa Kaunti ya Narok George Natembeya, ambaye anaongoza kikosi cha zaidi ya maafisa 200 wa usalama kutatua zogo hilo aliapa kutosaza yeyote.

“Kufikia sasa hutujapata jina la wanasiasa maarufu au mfanyabiashara mwenye ushawishi aliyehusika katika unyakuzi wa msitu huo,” alisema Bw Natambeya.

“Huu ni wakati wa kutenganisha siasa na uhifadhi wa mazingira. Tutafukuza yeyote asiye na stakabadhi za umiliki,” akaongeza Bw Natembeya.

Katika Msitu wa Maasai Mau, takriban ekari 29,000 zimetwaliwa na zaidi ya familia 2,500. Ripoti iliyowasilishwa bungeni iliorodhesha ekari 18,102 pekee za msitu zilizouzwa kiharamu

“Msimamo wa kweli na wa kisheria ni kuwa, serikali ya Kaunti ya Narok ndio pekee inahifadhi Maasai Mau kwa niaba ya jamii ya Maasai,”alisema Mbunge wa Narok Kusini Moitalel Ole Kenta.

Kati ya ekari 100,000 hadi ekari 400,000 zinakisiwa kugeuzwa makao ya watu katika Msitu wa Mau.

Ripoti hiyo ya 2009, iliwataja watu 25 wenye ushawishi mkubwa kisiasa ambao walipewa ekari 500 za msitu huo.