Habari

Serikali yatangaza Mei 25 sikukuu ya Eid al-Fitr

May 20th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

SERIKALI imetangaza Jumatatu Mei 25, 2020, kuwa itakuwa sikukuu ya mapumziko kote nchini wakati Waislamu wakitarajiwa kusherehekea sikukuu ya Idd ul-Fitr au Eid al-Fitr.

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i amechapisha siku hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali mnamo Jumatano.

“Umma unafahamishwa kwamba Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i anayehudumu katika serikali kuu, anatumia kifungu 2 (1) cha sheria za sikukuu ya kitaifa kutangaza Jumatatu ya Mei 25 kwamba ni sikukuu ya Idd ul-Fitr,” linasema chapisho hilo.

Sikukuu ya Idd huadhinishwa baada ya Waislamu kukamilisha siku 30 au 29 za mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kulingana na mwandamo wa mwezi.

Siku hiyo hutangulizwa kwa ibada misikitini au uwanja mkubwa kutokana idadi kubwa ya wanaojitokeza kwa swala.

Baada ya ibada, waumini husherehekea kwa kula pamoja na kuwanunulia jamaa zao zawadi na pia kuwafikia wasiojiweza katika jamii.

Hata hivyo, Idd ya mwaka huu itakuwa tofauti na ya miaka ya nyuma baada ya mataifa mengi kutikiswa na janga la virusi vya corona.

Familia nyingi zitalazimika kusherehekea nyumbani jinsi ambavyo wamekuwa wakiswali wakati wa Ramadhan baada ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko ya watu maeneo ya umma kama njia ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Ina maana mihemko, pilkapilka na hekaheka mijini na kazini zilizoandamana na siku hii ya kipekee, zitakosa mwaka huu.

Isitoshe, shughull nyingi za umma katika Kaunti za Kwale, Kilifi, Mombasa na Mandera ambazo zina wakazi wengi Waislamu pia zimezimwa baada ya serikali kupiga marufuku safari za kuingia au kutoka katika maeneo hayo.

Pia mtaa wa Eastleigh, Nairobi ambao umekuwa kitovu cha kibiashara ambako jamaa na marafiki hununulia familia zao zawadi siku hii pia imefungwa baada ya kurekodi maambukizi ya juu ya virusi vya corona.