Serikali yatangaza mikakati ya kuboresha sekta ya bodaboda

Serikali yatangaza mikakati ya kuboresha sekta ya bodaboda

Na WANGU KANURI

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i amewaeleza waendeshaji bodaboda wachukue leseni mpya kuanzia Machi 21.

“Shughuli za upatianaji leseni zitaendeshwa kwa siku 60 bila ya kuwatoza ada ya Sh5,000. Baada ya siku hizo 60 kukamilika, hakikisha kuwa una leseni ya kiteknolojia ya uendeshaji pikipiki,” akasema.

Akizungumza kwenye kikao na viongozi, Dkt Matiangi pia alisema kuwa wahudumu hao wa bodaboda watasajiliwa kwenye Vyama vya Ushirika (SACCO) na kuchunguzwa upya na wasimamizi wa maeneo na kaunti.

“Kunao wana rekodi kwenye Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI), tutaanza kuwachunguza ili tuwaondoe wanaotuharibia sifa,” akaongeza.

Maafisa kutoka Idara ya Kitaifa ya Usimamizi wa Serikali (NGAOs) pia watatarajiwa kufanya mikutano ya kila mwezi na wakuu wa waendeshaji bodaboda katika kila eneo.

Masharti haya yanatokea siku chache baada ya afisa wa Ubalozi wa Zimbabwe Tafadzwa Esnathi Chiposi kudhulumiwa kijinsia na kuibiwa simu iliyo na thamani ya Sh130,000.

Kudhulumiwa kwake kuliibua hisia kali miongoni mwa Wakenya huku likianika uozo uliokithiri katika sekta ya bodaboda.

Alhamisi wahudumu boda boda 16 walishtakiwa kufuatia unyama uliofanyika katika barabara ya Wangari Maathai almaarufu Forest Road.

You can share this post!

Chama cha Kanu chazindua manifesto yenye nguzo tano kuu

Takwimu za wasichana na akina mama wanaokeketwa Tharaka...

T L