Habari Mseto

Serikali yatia breki uajiri wa mameneja wakuu IEBC

April 29th, 2018 2 min read

Na MWANDISHIW WETU

WIZARA ya Fedha imesitisha shughuli ya kuajiriwa kwa mameneja wapya wa ngazi ya juu katika Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambao wangejaza nafasi ya waliostaafu au kufutwa.

Kwenye barua kwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Marjan Hussein Marjan, Katibu wa Wizara hiyo Kamau Thugge alisema tume hiyo haijapata idhini ya kuiwezesha kuendelea na zoezi hilo.

Dkt Thugge alisema IEBC ilifeli kuzingatia amri ya wizara yake iliyosimamisha shughuli zote za uajiri wa wafanyakazi wa umma kulingana na arifa yake nambari 2/2018.

“Kwa kuzingatia mahitaji makali kwenye makadirio ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2018/19, bajeti ya katikati ya muhula na hali kwamba uchaguzi mkuu umemalizika, tunapendekeza kuwa IEBC ifanye ukadiriaji wa majukumu kubaini majukumu ya nyadhifa hizo mpya,” Dkt Thugge akasema.

Barua hiyo inaendelea kusema: “IEBC pia inapasa kutumia zoezi hilo la ukadiriaji thamani ya kazi kupunguza idadi ya wafanyakazi wa kudumu kwa kuajiri vibarua, panapowezekana, haswa nyakati za uchaguzi mkuu.”

Mnamo Aprili 11, IEBC ilitangaza nafasi za wakurugenzi watatu (wa Masuala ya Wafanyakazi, Masaula ya Sheria na Uagizaji bidhaa na huduma) siku chache baada ya Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba kupewa likizo ya lazima ya miezi mitatu.

Watu waliohitimu kwa nyadhifa hizo walishauriwa kuwasilisha barua zao za maombi ya kazi kupitia tovuti ya ajira ya tume hiyo.

Wakati huo huo, IEBC imekanusha habari kwamba maafisa wanaohudumu katika afisa ya Afisa Mkuu Mtendaji wamepewa likizo ya lazima.

Kwenye taarifa katika ukurasa wake wa twitter, idara ya mawasiliano ya umma ya tume hiyo inasema maafisa hao walipewa majukumu mengine bali hawakufutwa.

“Na endapo walienda likizo ilikuwa ni likizo yao ya kawaida bali sio likizo ya lazima kama ilivyoripotiwa Jumamosi katika vyombo vya habari. Huenda wengine pia waliamua kupumzika kufikia siku ambazo hawakuwa wameenda likizo,” IEBC ikasema. Ilisemekana kuwa maafisa watano ambao walikuwa wakifanyakazi kwa karibu zaidi na Bw Chiloba waliagizwa kuondoka kupitia amri ya mdomo.

Wao ni; makarani wawili, wasaidizi wa kibinafsi wawili na tarishi mmoja waliamriwa waondoke katika kile kinachofasiriwa kuwa harakati za kuwang’oa washirika wa Bw Chiloba.

Amri hiyo ilitolewa na kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Bw Marjan Hussein Marjan.