Habari Mseto

Hakikisho ukuta wa Shimoni hautawaathiri wakazi

March 26th, 2019 2 min read

Na SAMUEL BAYA

NAIBU kamishna wa Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale Bw Josphat Biwott, amewahakikishia wakazi wa Shimoni kuwa ukuta unaojengwa ufuoni katika jeti ya Shimoni hautawaathiri.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu, Bw Biwott alisema wakazi watashirikishwa kuanzia mwanzo hadi mwisho.

“Hata hivyo, kwa sababu ya wasiwasi ambao umewaingia wakazi na hasa wavuvi kwamba huenda tutaziba njia ya kuelekea baharini, naomba kuwaeleza kwamba hilo halitafanyika kamwe,” akasema.

Ukuta huo unajengwa ili kuziba mianya ambayo alisema imekuwa ikitumiwa kufanya biashara za magendo ambazo zimegharimu serikali kodi ya fedha nyingi.

“Huu ukuta unajengwa na serikali kuu kupitia kwa halmashauri ya bandari nchini (KPA) kama njia mojawapo ya kukabiliana na biashara ya magendo ambayo imekuwa ikiendelea nyakati za usiku. Tunajua kuna watu ambao wamekuwa wakihepesha bidhaa kupitia kwa mianya iliyoko baharini na kupeleka hadi maeneo ya Wasini na visiwa vingine,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa tayari ameitisha kikao na wakazi siku ya Alhamisi ili kupeana mwongozo wa jinsi suala hilo litakavyoshughulikiwa ili kuridhisha pande zote mbili.

“Tunajua kumekuwa na baadhi ya makundi yanayodai kutetea haki za wakazi na ambayo yamekuwa yakipinga mradi huu. Tunachosema ni kuwa mradi huu ni muhimu sana sio kwa watu wachache ila kwa wakazi wengi wa Shimoni.

Baadhi ya bidhaa zinazopitishwa kimagendo hapa ni hatari na hivyo basi hatutaki wananchi wetu wahatarishiwe maisha,” akasema naibu huyo wa kamishna.

Wiki iliyopita, baadhi ya wakazi wa Shimoni walielezea hofu yao kuhusiana na ukuta huo ambao unanuiwa kujengwa katika eneo hilo wakisema kuwa utawaharibia shughuli zao za uvuvi.

Wakazi hao kupitia kwa kikundi cha Shimoni Development Initiative chini ya mwenyekiti wao Mohamed Shee walisema kuwa kama wenyeji, bado hawajashauriwa kuhusu ukuta huo.

“Sisi hatukuwa na habari hadi pale tulipoitwa na chifu wa Shimoni kuelezewa kuhusu mpango wa ujenzi wa ukuta. Tulishangaa sana kwa sababu mkutano wa baraza ulifaa uandaliwe mapema bila kuharakisha watu,” akasema Bw Shee.

Kulingana na wakazi hao, ujenzi wa ukuta huo unaanzia katika afisi za halmashauri ya utozaji kodi nchini (KRA) hadi katika egesho la wavuvi, umbali wa takrbani mita 900.

“Wasiwasi wetu mkuu ni kuwa ukuta huu huenda ukamaliza kabisa biashara yetu ya uvuvi. Pia tutakuwa na shida ya kufikia visiwa vya Wasini na Mkwiro,” akasema Bw Shee.

Aidha walisema kuwa baadhi ya vijiji ambavyo vitaathirika na ujenzi wa ukuta huo ni Majengo, Changaraweni, Anzwani, Kichaka Mkwaju, Mwazaru, Mbuyuni na Changai.

Mwenyekiti wa kikundi cha kusimamia mapango ya Shimoni Bw Hassan Juma alisema kuwa utawala katika eneo hilo uliwaambia wazi kwamba mradi huo utaendelea bila kipingamizi.

“Sasa ile picha ambayo tunapata ni kuwa tayari kila kitu kimemalizika na serikali imepanga kila kitu. Lakini kama wakazi, tunaamini kwamba tulifaa pia tuhusishwe katika mpango huu,” akasema.

Hata hivyo, naibu huyo wa kamishna alisema kuwa kumekuwa na vikao vya mara kwa mara kuhusiana na mpango huo ila baadhi ya makundi ya kutetea haki za jamii yamekuwa yakiwadanganya wananchi.