Serikali yatoa Sh17.4 bilioni kufadhili masomo katika shule zote za umma

Serikali yatoa Sh17.4 bilioni kufadhili masomo katika shule zote za umma

Na WINNIE ONYANDO

SERIKALI ilitoa Sh17.4 bilioni kama ufadhi wa masomo katika shule zote za umma nchini muhula huu wa kwanza.

Katika taarifa kwa wanahabari iliyotolewa Jumanne, Wizara ya Elimu ilisema kuwa Sh2.62 bilioni zitawafadhili wanafunzi katika shule za msingi huku Sh14.85 bilioni zikiwafadhili wanafunzi katika shule za upili.

Wizara pia ilieleza kuwa pesa hizo zilitolewa kuhakikisha kuwa masomo yanaenda kisawasawa katika shule zote za umma huku ikiwaomba walimu wakuu kuhakikisha kuwa masomo yanaendelea bila kukatizwa.

“Walimu wakuu wahakikishe kuwa wanafunzi wanatumia muda wao vizuri hasa katika muhula huu mfupi,” taarifa ikasoma.

Wizara iliwaomba walimu kushauriana na wazazi ambao watoto wao hawajamaliza kulipa karo ili kutafuta njia mbadala ya kukamilisha malipo.

Walimu wanaoenda kinyume na sheria ya Wizara ya Elimu kwa kuongeza karo kiholela watachukuliwa hatua.

Serikali iliwaomba wazazi na wadau husika kuhakikisha kuwa kila mtoto aliyefanya mtihani wa kitaifa ya KCPE kujiunga na kidato cha kwanza kwa kuwa tayari serikali imetoa ufadhili wa masomo.

You can share this post!

Viongozi wa OKA wataka Moi ataliki Uhuru ajiunge na...

Yego nje ya Olimpiki