Kimataifa

Serikali yatumia mamia ya mbuzi kuzuia moto kutokea

June 25th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

LISBON, URENO

SERIKALI imekodisha mamia ya mbuzi watakaotumiwa kuzuia majanga ya moto ambayo hutokea vichakani na kuenea hadi vijijini.

Hatua hii imechukuliwa baada ya kubainika kuwa idara ya zimamoto hulemewa kuzima mioto aina hiyo. Mwaka uliopita, moto ulioenea kutoka vichakani ulisababisha vifo vya watu 106.

Kwa kawaida, visa hivyo huibuka wakati wa kiangazi na sasa inatarajiwa mbuzi watatafuna nyasi na mimea mingine midogo ambayo hueneza moto kutoka kwa vichaka vya milimani.

Ripoti zinasema hii ni mara ya kwanza kwa Ureno kutumia mbinu hii ambayo imewahi kutumia katika nchi zingine kama vile Amerika.

Waziri msaidizi wa misitu na ustawishaji wa maeneo ya mashambani, Miguel Joao de Freitas, alinukuliwa kusema mbinu hii itatumiwa huku idara ya zimamoto ikizidi kuimarishwa kama vile kwa kunua vifaa zaidi vya kisasa.

“Mwaka uliopita tuligundua kwamba inafaa tuchukue hatua tofauti. Jambo muhimu la dharura zaidi ni kuzuia majanga, na hili linafaa kufanywa haraka iwezekanavyo,” akasema.

Wakazi wa vijiji ambavyo huathirika walipohojiwa walisema zamani kulikuwa na mbuzi wengi ambao walikuwa wakitafuna mimea hiyo inayoshika moto haraka inapokauka, lakini siku hizi vijana wamejitenga na ufugaji.

Hata hivyo, utafiti wa kisayansi unaonyesha kwamba moto huo ni miongoni mwa changamoto zinazokumba ulimwengu kutokana na ongezeko la joto duniani kufuatia uharibifu wa mazingira.

-Imekusanywa na Valentine Obara