Habari Mseto

Serikali yawazia kuagiza mahindi kutoka nje

May 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali juma hili itaamua ikiwa itaagiza mahindi kutoka nje kutokana kuwa mahindi yaliyomo nchini yanatarajiwa kuisha kufikia mwishoni mwa mwezi Juni.

Upungufu huo unawatia wengi kiwewe ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya wananchi hutegemea mahindi.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Kilimo Andrew Tuimur alisema mashirika husika ya serikali yatajadiliana kuhusiana na idadi ya magunia yatakayoagizwa kutoka nje na muda wa usafirishaji kwa lengo la kuepuka kuharakisha dakika ya mwisho mahindi yanapokuwa yakihitajika.

Watengenezaji wa unga wa mahindi na watengenezaji wa sera tayari wameonya kuwa mahindi yaliyoagizwa kutoka nje huchukua siku 45 kufika nchini.

Ikiwa muda mwingi utachukuliwa kuagiza, inamaanisha kuwa kutakuwa na upungufu wa mahindi nchini, hali inayoweza kuwafanya watu wengi kuathirika na njaa.

“Tunafanya uamuzi wiki hii kuhusiana na uagizaji wa mahindi. Tunahitaji kujua idadi kamili ya magunia yanayohitajika,” alisema Dkt Tuimur.

Kulingana naTimothy Njagi, mtafiti katika Taasisi ya Tegemeo, Chuo Kikuu cha Egerton, serikali inafaa kuharakisha kuagiza mahindi hayo kwa sababu ya muda unaochukuliwa kuyasafirisha kutoka ng’ambo hadi nchini.

“Tumechelewa kwa miezi miwili. Hii ina maana kuwa ikiwa utaratibu huo utaanza ukiwa umechelewa, mahindi hayo hayatatimiza lengo,” alisema Dkt Njagi.

Kulingana na mkurugenzi wa Tume ya Nafaka Afrika Mashariki Gerald Masila, uagizaji unafaa kuanza mara moja kutokana na kuwa mahindi yaliyomo nchini hayawezi kulisha wananchi zaidi ya Julai.