Habari

Serikali yawazia kuzuia matumizi ya mafuta taa

May 6th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

MAMILIONI ya Wakenya ambao hutegemea mafuta ya taa kwa kupika na kupata mwangaza huenda wakalazimika kutumia mbinu nyingine baada ya Mamlaka ya Kudhibiti Kawi nchini (ERC) kupendekeza kuondoa bidhaa hiyo sokoni.

ERC inasema kuwa utumiaji wa mafuta ya taa nchini umezidi na kuzidisha madhara yake kwa watu na mazingira, na hivyo inataka kupandisha bei yake kufikia ile ya mafuta ya dizeli kama mbinu ya kuwafanya Wakenya kutoyanunua.

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Pavel Oimeke Jumamosi alieleza Taifa Leo kuwa kutokana na bei ya chini ya mafuta taa, wauzaji watundu wamekuwa wakichanganya bidhaa hiyo na mafuta ya dizeli na kuwauzia watumizi wa magari, jambo linaloharibu injini za magari.

Bw Oimeke, ambaye alikuwa akizungumza katika kongamano la kujadili masuala ya kawi na watumizi, alisema utundu huo umeharibia Kenya biashara ya diseli na mataifa ya nje kama Uganda, Rwanda, Burundi na sehemu za Tanzania ambayo sasa yamechoshwa na kuuziwa mafuta machafu.

“Mamlaka imekuwa ikishauriana na wizara ya fedha na ya kawi kwa nia ya kushinda changamoto ya kuchafuliwa kwa mafuta. Kwa sasa Kenya inatumia lita milioni 33 za mafuta taa japo inafaa kuwa chini ya lita milioni 5 kwa mwezi,” akasema Bw Oimeke.

Alisema, hata hivyo kuwa lita milioni 27 huishia kutumiwa na magari kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuchanganya na mafuta ya diseli na hivyo kuharibu magari kwa wingi.

Bw Oimeke alitaja bei ya chini ya mafuta taa kuwa sababu ya utumizi huo mkubwa, na hivyo akasema ERC imeamua kuongeza bei ya mafuta taa ili kutoa suluhu.

“Tunataka serikali kuongeza ushuru kwa mafuta taa badala ya bidhaa nyingine za petroli, ili kuokoa Sh34 billioni za ushuru tunaopata kutoka mataifa ya nje, kuokoa misitu na afya ya Wakenya,” akasema Bw Oimeke.

Hata hivyo, Wakenya watapewa mbinu mbadala kama mpango wa gesi za bei rahisi pamoja na taa zinazotumia nguvu za jua zilizopunguzwa bei na serikali.

Katibu Mkuu wa muungano wa watumizi wa bidhaa (Cofek) nchini Stephen Mutoro alisema kuwa japo wazo la ERC litasaidia kutetea mazingira na afya ya wakenya, ni vyema hatua zichukuliwe kwa mpangilio ili kuzuia kuwaumiza watumizi wa bidhaa hiyo.

“Tunakubaliana na mdhibiti wa kawi lakini hatua hizo sharti zichukuliwe kwa mpangilio,” akasema Bw Mutoro.