Michezo

Serikali yazidi kuzembea kutoa fedha kwa Harambee Stars kusafiri Ethiopia

September 26th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

ZIKIWA zimesalia siku 15 tu kabla mechi ya kufuzu kushiriki dimba la Bara Afrika mwaka wa 2019 (Afcon) kati ya Kenya na Ethiopia, serikali bado haijatoa Sh26 milioni zinazohitajika kwa matayarisho ya mechi hiyo.

Kikosi cha timu ya Taifa, Harambee Stars kinafaa kusafiri hadi mji wa Bahir Dar Oktoba 10 kukabiliana na Ethiopia kisha timu hizo mbili zirudiane siku tatu baadaye, Oktoba 14 katika uga wa MISC Kasarani.

Ingawa kocha Sebastien Migne amekitaja kikosi cha muda cha wachezaji wanaofaa kuwajibikia mechi hiyo, huenda ukosefu wa fedha ukawa kikwazo kikuu katika mchakato mzima wa matayarisho.

Shirikisho la soka nchini(FKF) lilikuwa limekadiria bajeti ya Sh26 milioni kugharamia mikondo mikili ya mechi hiyo lakini sasa FKF haijapokea mawasiliano yoyote au ithibati kutoka wizara ya michezo kwamba pesa hizo zitatolewa.

“Tumekwama na hatuwezi kuendelea na matayarisho ilhali hatuma fedha. Kila kitu sasa kinaenda tenge,” akasema afisa moja wa FKF asiyetaka jina lake linukuliwe kwa kuwa si msemaji wa shirikisho hilo.

Kulingana na afisa huyo, haijulikani ni lini wachezaji wanaosakata soka ya kulipwa nje ya nchi wataanza kuwasili kwasababu hawajalipiwa tiketi za safari zao huku timu ikikosa kuandaa kambi ya mazoezi kwa ukosefu uo huo wa ngwenje.

Vile vile taarifa zimechipuka kwamba kocha Migne hajalipwa mishahara ya miezi miwili nazo Sh19milioni zilizotumika kuandaa mechi ya Afcon dhidi ya Ghana na ya kirafiki dhidi ya Malawi mwezi wa Agosti bado hazitolewa wala kulipwa.

“Pesa za mechi ya Ghana hazijatolewa na tunalazimika kusubiri fedha za mechi ya Ethiopia. Mambo ni magumu,” akaongeza Afisa huyo.

Kenya walifufua matumaini yao ya kufuzu kipute hicho cha mwaka wa 2019 baada ya kuitandika Black Stars 1-0 kwenye mechi ya Kundi F iliyoandaliwa uga wa Kasarani.