Serikali yazima Mt Kenya TV kwa kupotosha watoto

Serikali yazima Mt Kenya TV kwa kupotosha watoto

Na SAMMY WAWERU

MAWIMBI ya runinga ya Mt Kenya inayomilikiwa na M/s Slopes Media House Ltd Jumatano yameondolewa hewani kwa kupeperusha programu chafu ya kupotosha watoto.

Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA) imetoa taarifa ya kufunga kituo hicho kwa muda wa miezi minne, kufuatia kipindi kilichopeperushwa na ambacho kimetajwa kuwa na jumbe za ngono, matumizi ya dawa za kulevya, wizi na dhuluma za kijinsia.

Kwenye programu ya ‘Mucii Ciiana’ yenye mada ‘Jimmy’, Mt Kenya imesemekana kupeperusha matini yenye jumbe hizo chafu muda usiofaa, wakati watoto wengi huwa hawajalala.

“Mamlaka imegundua runinga hiyo ilipeperusha kontenti inayopaswa kutazamwa na watu wazima, saa zisizofaa na wakati wa likizo wanafunzi wakiwa nyumbani. Hatua hiyo iliwaweka katika hatari ya kuwapotosha kwa kontenti chafu,” CA ikaelezea kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Mamlaka hiyo ya mawasiliano nchini ilichukua hatua hiyo kufuatia malalamishi ya umma mitandaoni.

Kutokana na uchunguzi, Mt Kenya TV imepatikana na hatia ya kukiuka kifungu cha 83A cha Sheria za Habari na Mawasiliano nchini.

Aidha, CA imesema kontenti iliyopeperushwa haijaafikia ubora na matakwa ya Bodi ya Kutathmini Filamu Nchini (KFCB).

“Baada ya kupatikana na hatia runinga hiyo imepokezwa adhabu ya kutopeperusha matangazo yake kwa muda wa siku 120,” CA ikasema.

Runinga ya Mt Kenya pia imepigwa faini ya Sh500, 000. Pia imepewa makataa ya siku saba kutathmini utendakazi katika chumba cha habari, programu, na pia wafanyakazi wake kupitia mafunzo ya utangazaji bora.

Aidha, imetakiwa kuhakikisha watangazaji na maripota wake wote wamepata idhini ya Baraza la Vyombo vya Habari Nchini (MCK) kuwa katika nyanja ya uanahabari, kati ya mahitaji mengineyo.

You can share this post!

Jina la Martha Koome latua bungeni

Mombasa Cement na NMG zashirikiana kuinua elimu Kilifi...