Serikali yazima wafu kuzikwa usiku

Serikali yazima wafu kuzikwa usiku

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI za kaunti zinafaa kuruhusu watu wanaokufa kutokana na virusi vya corona kupatiwa mazishi ya heshima badala ya kuzikwa usiku, Wizara ya Afya imesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt Patrick Amoth, alisema japo ni lazima kanuni za kuzuia maambukizi ya corona zizingatiwe kikamilifu, kuzika miili usiku ni kukosea marehemu heshima.

“Kanuni zilitolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) za kuzika miili ya wanaokufa kutokana na corona zinafaa kuzingatiwa wakati wa mazishi. Lakini tunahimiza serikali za kaunti kukoma kuzika miili usiku. Zipatie jamaa wa marehemu fursa ya kuandaa mazishi ya heshima,” alisema Dkt Amoth akiwa katika hospitali ya Othaya, Kaunti ya Nyeri.

Dkt Amoth alikuwa ameandamana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kukagua maandalizi ya kukabiliana na janga la corona kaytika kaunti hiyo.

Hata hivyo alisema desturi za kitamaduni zinazoweza kusambaza virusi hivyo hazitaruhusiwa.

Baadhi ya serikali za kaunti zimeagiza mazishi kufanyika saa 24 baada ya kifo kutokea.

Madai ya ubaguzi yameibuka huku baadhi ya waathiriwa wakizikwa usiku na jamaa zao kunyimwa nafasi ya kuhudhuria huku ya wengine yakifanyika mchana na kuhudhuriwa na mamia ya watu.

Dkt Amoth alihimiza watu kuripoti kisa chochote cha dhuluma na ukiukaji wa kanuni hizo.

Kwa mara nyingine, Bw Kagwe alionya wanasiasa na viongozi wengine dhidi ya kukiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona na kuwataka machifu kuhakikisha kuwa hakuna mikutano ya hadhara katika maeneo yao.

Bw Kagwe alisema mbali na corona, serikali inakabiliana na ongezeko la maradhi yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani, msukumo wa damu na kisukari.

“Mzigo wa maradhi yasiyo ya kumbukizana ungali unaongezeka na kutia wasiwasi. Watu walio na maradhi haya huwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa corona, na kuna haja ya kukaguliwa mapema ili kupata matibabu,” alisema Waziri Kagwe.

Alitoa mfano wa saratani akisema inaua watu 32, 000 kila mwaka. Jana, visa vipya 132 vya corona vilithibitishwa nchini na kufikisha idadi ya maambukizi kuwa 3167. Hospitali ya Othaya iliyo chini ya hospitali ya kitaifa ya Kenyatta inatarajiwa kuwa kituo cha kushughulikia wagonjwa wa corona kaunti ya Nyeri. Visa tisa vimethitishwa katika kaunti hiyo.

You can share this post!

Pigo kwa familia korti kuikataza kuzika jamaa wake upya

14 waliotangamana na aliyeugua corona watupwa kwa karantini

adminleo