Habari za Kitaifa

Serikali yazinduka baada ya mkasa jijini

February 4th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI ilionekana kuanza kugutuka Jumamosi ilipowasimamisha kazi maafisa wanne wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (Nema) kuhusiana na mlipuko wa gesi uliosababisha maafa katika eneo la Embakasi, Nairobi Alhamisi usiku.

Hatua hiyo ilichukuliwa saa chache baada ya Rais William Ruto kuamuru kufutwa kazi na kushtakiwa kwa maafisa waliotoa leseni kwa biashara ya gesi eneo hilo kinyume cha sheria.

Watu watatu walipoteza maisha na wengine 280 wakajeruhiwa vibaya katika mkasa huo uliotokea katika eneo la Mradi Village katika eneobunge la Embakasi Mashariki.

“Baada ya kufanya ukaguzi wa kina wa taratibu za utoaji leseni, Bodi ya Usimamizi imebaini dosari kadha katika utoaji leseni kwa kiwanda cha gesi ambako mkasa huo uliotokea. Imethibitishwa kwamba, maafisa wanne walitoa leseni hiyo kinyume cha sheria licha ya kampuni hiyo kutozingatia masharti hitajika,” mwenyekiti wa bodi ya Nema Emilio Mugo alisema kwenye taarifa.

“Kwa hivyo, bodi imeamuru maafisa wahusika waondoke afisini mara moja hadi uchunguzi unaoendeshwa na asasi husika za serikali utakapokamilika,” akaongeza.

Kulingana na Nema, waliosimamishwa kazi ni pamoja na; Mkurugenzi wa kitengo cha uzingativu wa sheria za mazingira, naibu wake na maafisa wawili katika kitengo cha ukaguzi wa athari za miradi kwa mazingira (EIA).

Hatua hiyo imejiri saa chache baada ya Rais Ruto kuagiza Wizara ya Kawi kuwapiga kalamu maafisa waliohusika na utoaji wa leseni kwa kiwanda hicho.

Akiongea Jumamosi asubuhi katika eneobunge la Lugari, Kaunti ya Kakamega, Dkt Ruto alisema hatua hiyo ilichangiwa na ufisadi, utovu wa maadili na ulafi miongoni mwa maafisa husika wa serikali.

“Kule Nairobi, kulitokea mlipuko wa gesi na watu wakakufa na wengine wengi wakajeruhiwa. Hii ilichangiwa na uzembe na ufisadi wa maafisa wa serikali ambao walitoa leseni kwa kiwanda hicho katika eneo la makazi,” akasema alipohutubia wananchi baada ya kuzindua mradi wa ujenzi wa soko jipya katika kituo cha biashara cha Chekalini.

“Kwa hivyo, nimeagiza Wizara ya Kawi kwamba, maafisa wote waliotoa leseni hiyo baada ya wao kuhongwa wafutwe kazi leo na wasukumwe gerezani kwa makosa waliyotenda,” akaongeza.

Rais Ruto alisema hamna haja kwa maafisa kama hao kuendelea kushikilia nyadhifa serikalini na kulipwa mishahara kutokana na pesa za walipa ushuru.

Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta Nchini (Epra) ndio yenye mamlaka kisheria kutoa kibali kwa biashara za aina zozote za kawi nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Epra ni Daniel Kiptoo.

Mnamo Ijumaa, Epra ilisema ilikataa kutoa kibali kwa mmiliki wa kiwanda hicho mara tatu mwaka 2023.

Asasi hiyo ilisema haikukubaliana na wazo la mfanyabiashara huyo kuanzisha kiwanda cha gesi ya kupikia katika eneo la makazi.

“Maombi ya kusaka kibali cha kuanzisha kiwanda cha gesi eneo hili yalipokewa na Epra mnamo Machi 19, 2023, Juni 20, 2023 na Julai 31, 2023. Maombi yote yalikataliwa kwa sababu hayakufikia masharti hitajika kuanzisha kituo cha kuhifadhi na kujaza gesi katika eneo hili,” Epra ikasema kwenye taarifa.