HabariSiasa

Serikali za kaunti kupokea Sh50 bilioni Ijumaa

September 17th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI 47 za kaunti sasa zitaanza kupokea Sh50 bilioni kutoka Hazina ya Kitaifa kuanzia Ijumaa wiki hii, kaimu waziri wa Fedha Ukur Yatan ametangaza.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini Mswada wa Ugavi wa Mapato (DoRB) wa 2019 Jumanne uliopitishwa baada ya Bunge la Kitaifa na Seneti kukubaliana kuhusu kiasi cha fedha kinachopasa kutengewa serikali za kaunti katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

Kulingana na mswada huo, kaunti zimetengewa jumla ya Sh378.1 bilioni, Sh316.5 bilioni zikiwa ni sehemu ya mapato yaliyokusanywa kitaifa huku Sh61.6 zikiwa fedha zilizotengwa mahususi kwa majukumu mahususi katika kaunti.

“Kufuatia kutiwa saini kwa mswada wa ugavi wa mapato leo asubuhi na Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta, Hazina ya Kitaifa imewatumia zaidi ya Sh50 bilioni kwa serikali za kaunti. Pesa hizo ni mgao wa miezi ya Julai na Agosti uliocheleweshwa kufuatia mvutano kuhusu mswada huo,” akasema Bw Yatani.

“Hata hivyo, pesa hizo zitafika katika kaunti za serikali hizo kuanzia Ijumaa wiki hii baada ya bunge la kitaifa na seneti kupitisha mswada wa ugavi wa mapato baina ya kaunti (CARB),” akaongeza kwenye kikao na wanahabari afisini mwake Nairobi.

Bw Yatani alikuwa ameandamana na Katibu wa Idara ya Mipango katika Wizara yake Julius Muia, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) James Gathii Mburu na kaimu msimamizi wa bajeti Stephen Masha.

Alisema amepokea ujumbe kutoka kwa Seneti kwamba mswada wa CARB ungepitishwa Jumanne katika vikao vyake vinavyoendelea Kitui.

Na kwa upande wake, Bunge la Kitaifa linatarajiwa kuupitisha mswada huo leo, kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta auitie sahihi.

Bw Yatani, aliahidi kwamba Hazina ya Kitaifa itawasilisha mgao wa mwezi Sepetemba kwa kaunti kuanzia Oktoba mwaka huu.

“Tunaamini kwamba kuanzia Ijumaa serikali zote za kaunti zitaweza kuwalipa wafanyakazi wao mishahara ambayo imecheleweshwa kwa zaidi ya miezi miwili. Na kuanzia mwezi ujao tutahakikisha kuwa tunatuma pesa kwa kaunti bila kucheleweshwa kulingana na kipengee cha 219 cha Katiba na sehemu ya 17 (7) ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, 2012 ili ziweze kuendelea kutoa huduma,” akasema.

Baada ya kutia saini mswada wa DoRB jana asubuhi Rais alizitakana serikali za kaunti kuweka mikakati bora ya kuziwezesha kukusanya mapato yao ili zisiwe zikitegemea pesa kutoka Hazina ya Kitaifa nyakati zote.

“Nazitaka serikali zote za kaunti zianzishe mifumo bora ya kuziwezesha kukusanya mapato mengi kutokana na kodi, na ada mbalimbali zinazotoza. Mapato haya yataziwezesha kugharamia mahitaji ya dharura kama ulipaji mishahara huku pesa kutoka Hazina Kuu zikitumiwa kufadhili miradi ya maendeleo,” Rais Kenyatta akasema.

Kutiwa saini kwa mswada huo kunafuatia muafaka uliopatikana kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa kwamba kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni katika mwaka huu wa kifedha ulioanza Julai 1.

Kwa muda wa miezi miwili wabunge na maseneta wamekuwa wakivutaka kuhusu suala hilo.

Maseneta walipendekeza mgao wa Sh335.7 bilioni, kiasi ambacho kilifikiwa na Tume ya Ugavi wa Rasilimali (CRA). Hata hivyo, wabunge walishikilia kiasi cha Sh316.6 bilioni msimamo ambao uliungwa mkono na Rais Kenyatta.

Lakini majuma mawili yaliyopita maseneta walilegeza msimamo baada ya magavana kutisha kusitisha shughuli katika kaunti endapo mvutano huo utaendelea baada ya Septemba 17.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen alisema “tumefanya uamuzi huo mchunguili kuzuia uwezekano wa kusitishwa kwa shughuli katika kaunti”.

“Fedha hizo hazitoshi, lakini ni afadhali na seneti itaendelea kuendelea kupigania fedha zaidi wakati mwingine. Seneti haitaruhusu ugatuzi ambao ndio nguzo kuu ya Katiba yetu kuhujumiwa kupitia njama fulani,” Bw Murkomen akasema.

Mvutano umekuwa ukiendelea kuhusu suala hilo tangu mwezi Juni hali iliyopelekea bajeti ya mwaka huu kusomwa kabla ya kupitishwa kwa mswada wa ugavi wa fedha.