Makala

Serikali za kaunti zarudishiwa magari hewa, zikilazimika kuyatafuta yaliyopotea

May 12th, 2024 3 min read

NA MAUREEN ONGALA

MASWALI yameibuka kuhusu yaliko magari yaliyokuwa yakitumika na manispaa mbalimbali nchini, mchakato wa kukabidhi mali hizo kwa serikali za kaunti ukiendelea nchini.

Mbali na magari, pia kuna changamoto kuhusu ardhi inayomilikiwa na serikali.

Kamati ya Ushirikiano wa Serikali Kuu na Serikali za Kaunti (IGRTC) imesema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya ardhi inayomilikiwa na serikali nchini haina hatimiliki na imenyakuliwa na watu wanaodai ndio wamiliki halisi.

Mjini Kilifi, asilimia 97 ya ardhi ya serikali haina stakabadhi hitajika na imevamiwa na maskwota.

Afisa Mkuu Mtendaji wa IGRTC Dkt Kipkurui Chepkwony aliambia wanahabari kwamba kamati yake inashirikiana na Wizara ya Ardhi na wizara nyingine na asasi husika kupata stakabadhi na taarifa nyingine muhimu za mali zinazofaa kukabidhiwa kwa kaunti.

Kaunti ya Kilifi ilipokea takriban magari kadhaa na hatimiliki za vipande viwili vya ardhi.

“Ardhi ya umma, iwe ni ardhi ya jamii, ya serikali ya kitaifa au ya serikali ya kaunti inajulikana na kutambulika. Tatizo tu ni washikilizi wa sasa wa ofisi hizo. Asilimia kubwa ya ardhi ya umma haijawahi kurekodiwa hapo awali au hatimiliki zake kutengenezwa,” akasema Dkt Chepkwony.

Dkt Chepkwony alisema kamati yake inafanya kazi na Wizara ya Ardhi na Tume ya Kitaifa ya Ardhi ili kutwaa na kuweka kumbukumbu za ardhi hiyo.

“Wizara na NLC zimesema mashamba yote haya yanatambulika na tunachofanya sasa ni kuyakadiria thamini, kuyatambua na kuhamisha umiliki ambao ulikuwa wa Serikali ya Kitaifa hadi kwa serikali za kaunti,” alisema.

Alisema hakuna ardhi itakayopotea na kuna taratibu za kuirejesha inayokaliwa kinyume cha sheria.

Kilifi ilikabidhiwa ardhi ya Huduma za Mifugo na nyingine ya Maendeleo ya Kijamii.

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alisema kuwa Serikali ya Kaunti itajenga Makao Makuu ya Kaunti hiyo katika ardhi ya Huduma za Maendeleo ya Kijamii kwa Sh500 milioni.

“Ardhi ya Huduma za Maendeleo ya Kijamii ni ardhi ya umma na mtu yeyote anayedai kuwa na hati zake ni bandia. Tumetenga Sh270 milioni kati ya Sh500 milioni na tuko tayari kuanza mradi,” akasema gavana Mung’aro.

Gavana Mung’aro alisema hivi karibuni, serikali ya kaunti itaanza ujenzi wa makazi ya Naibu Gavana katika ardhi ya Huduma za Mifugo.

“Tunafurahi kupata vipande hivi kwa sababu imekuwa ndoto yetu. Vipande hivi vya ardhi ni muhimu kwa serikali ya kaunti ya Kilifi na ni miongoni mwa mashamba ya umma 1228 ambayo mengi yamenyakuliwa,” akasema.

Alisema serikali ya Kaunti itatumia mbinu mbili katika kurejesha mashamba hayo.

Mbinu ya kwanza ni kutwaa mali hiyo moja kwa moja nay a pili ni kuwataka maskwota kuinunua ardhi wanayokalia la sivyo wafurushwe.

Alisema zingatio litakuwa kujenga ofisi za umma kwa ardhi inayorejeshwa.

“Vipande hivi viwili ambavyo tumekabidhiwa ni vya thamani ya Sh700 milioni,” alisema.

Baadhi ya ardhi zilizonyakuliwa za serikali huko Kilifi ni pamoja na ile ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kilifi huko Mkwajuni ambayo imekaliwa na maelfu ya maskwota.

Hata hivyo, kulikuwa na utata wakati wa kukabidhiwa mali baada ya Gavana Mung’aro kutangaza kuwa magari mengi hayakuwepo.

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro akiweka nambari za usajili kwa gari la kaunti. PICHA | HISANI

Bw Mung’aro alifichua kuwa Serikali ya Kaunti haijapokea magari 259 yenye thamani ya Sh51 milioni kutoka kwa Serikali ya Kitaifa kama ilivyoelezwa na IGRTC.

“Kwa mujibu wa ripoti ya Afisa Mkuu Mtendaji wa IGRTC, tunatakiwa kuwa na magari 259 lakini nataka nyinyi wanahabari mtoe taarifa kuwa sio yote yaliyorejeshwa. Kuna magari ambayo kamati haikuyaona ilipokuwa ikizunguka,” akafichua.

Gavana Mung’aro alisema serikali ya kaunti ina jukumu la kutafuta magari hayo.

Ingawa hivyo, hakufichua ni magari mangapi ambayo serikali ya Kaunti ilikuwa imekabidhiwa na IGRTC, ingawa mwandishi wa Taifa Jumapili alihesabu magari sita.

“Itatulazimu kufuatilia kujua kwa kurejelea madaftari ya serikali ili kujua ni magari mangapi yanapatikana, ni mangapi yenye hitilafu za kimitambo na yapo kwenye karakana, na ni mangapi ambayo haifai kuwa barabarani ili yauzwe kama vyuma chakavu,” alisema.

Bw Mung’aro alisema magari ambayo serikali ya kaunti itarekebisha bado yanafaa barabarani kusaidia katika utoaji wa huduma.

Awali, Dkt Chepkwony alikuwa amesema kuwa IGRTC ilikuwa ikikabidhi magari 259 kwa Kaunti ya Kilifi.

“Tunakabidhi jumla ya magari 259 ambayo ni mali inayohamishika, kwa Kaunti ya Kilifi. Ni yenye thamani ya hadi Sh51 milioni na huu ni mchakato ulioanza tangu wakati wa mamlaka ya mpito na tuna furaha kama IGRTC kukabidhi mali hizi,” akasema.

Dkt Chepkwony alisema kuwa kukabidhi mali hizo kwa kaunti kutashughulikia masuala matatu, ikiwa ni pamoja na suala la ukaguzi wa mali na kusaidia katika kuhakikisha kaunti zinabuni rejista yao ya mali zinazosimamia.

Pia, serikali za kaunti zingezingatia mtindo huo mpya ili kuwa na sajili hitajika ya mali.

Alisema wameanza mchakato huo na serikali 41 za kaunti.

“Kuanzia 2013, serikali za Kaunti zimekuwa zikipata ugumu wakati wa ukaguzi kutokana na suala la matumizi ya magari ambayo hayako katika majina yao na pia hazikuwa na sajili ya mali,” alisema.

Hafla hiyo ilifanyika katika makazi ya Gavana wa Kilifi mjini Kilifi.

Kamishna wa kaunti ya Kilifi Josephat Biwott alikuwepo.