Habari Mseto

Serikali za kaunti zatakiwa zikabidhi mahakama za manispaa kwa idara ya mahakama

November 13th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

SERIKALI za kaunti zimetakiwa kuzikabidhi mahakama za manispaa kwa idara ya mahakama kama mojawapo ya njia za kuzipunguzia mzigo serikali za kaunti.

Kulingana na Naibu Rais, hatua hii ni kutokana na makubaliano kati ya serikali za kaunti na Jaji Mkuu.

Bw Ruto alisema kuwa hatua hii itahakikisha mahakama za manispaa zinafanya kazi kwa utaalamu zaidi.

“Makubaliano hayo ni pamoja na jinsi ya kusimamia mahakama hizo,” akasema Bw Ruto.

Naibu Rais alizungumza baada ya kukutana na Baraza Shirikishi la Bajeti na Masuala ya Uchumi – Intergovernmental Budget and Economic Council (IBEC) – katika makao rasmi ya Naibu Rais mtaani Karen.

Aliongeza kuwa mahakama za manispaa ambazo zinahudumu katika majengo ya kaunti zitaendelea kuhudumu bila ya idara ya mahakama kulipishwa kodi yoyote.

Hii ilijiri wakati serikali za kaunti zilipata pigo baada ya pendekezo la kuchukua mikopo ya muda mfupi (short-term loans).

Naibu Rais alisema kuwa hatua hiyo ni kufuatia makubaliano kati ya mataifa ya Afrika Mashariki kuwa mataifa yake hayataweza kuchukua mikopo kutoka kwa benki kuu za mataifa yao.

“Mataifa ya Afrika Mashariki yamekubaliana kuwa serikali hazitaweza tena kuchukua mikopo kutoka kwa benki kuu. Hatua hii inatarajiwa kuchukua mkondo kuanzia mwaka 2021,” akasema Ruto.

Akaongeza: “Kutupiliwa mbali kwa ombi hilo ni kwa sababu serikali kuu iko katika hatua ya kujiondoa kutoka kwa uombaji fedha kutoka kwa benki kuu.”