Michezo

Sevila yailazimishia Barca sare

June 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BARCELONA walipoteza alama mbili muhimu katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Juni 19, 2020 baada ya kulazimishiwa sare tasa na Sevilla uwanjani Ramon Sanchez-Pizjuan.

Matokeo hayo yaliweka wazi vita vya kuwania ubingwa wa kipute hicho msimu huu huku Barcelona kwa sasa wakijipata katika hatari ya kupitwa na washindani wao wakuu Real Madrid.

Kabla ya Real kuvaana na Sociedad mnamo Juni 20, kikosi hicho cha kocha Zinedine Zidane kilikuwa kikijivunia alama 62, tatu pekee nyuma ya Barcelona ambao ni watetezi wa taji la La Liga.

Licha ya Barcelona kutamalaki mchezo katika kipindi cha kwanza kilichoshuhudia fataki ya nahodha na mvamizi Lionel Messi ikibusu mwamba wa goli la wenyeji, Sevilla walirejelea kipindi cha pili kwa matao ya juu na kuwazidi maarifa wanasoka wa kocha Quique Setien katika takriban kila idara.

Uthabiti wa ulinzi wa Sevilla ulihangaisha safu ya mbele ya Barcelona iliyokuwa chini ya uongozi wa Messi, Luis Suarez, Martin Braithwaite na Antoine Griezmann.

Aidha, kasi ya mshambuliaji Lucas Ocampos wa Sevilla iliwakosesha amani mabeki Clement Lenglet, Nelson Semedo na Gerrard Pique wa Barcelona. Ushirikiano mkubwa kati ya Ocampos na fowadi Munir El Haddadi ulimweka kipa Marc-Andre Ter Stegen wa Barcelona katika ulazima wa kusalia macho katika kipindi kizima cha pili.

Sevilla walibana sana safu yao ya ulinzi huku wakisalia na mabeki watano kila mara walipopoteza mpira. Mbinu yao hiyo iliwazalia matunda – alama moja ambayo iliwasaza katika nafasi ya tatu kwa alama 52 kadri wanavyopania kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Katika kipindi cha pili, mpira wa ikabu uliochanjwa na Messi katika dakika ya 79 ndiyo fursa ya pekee ambayo Barcelona walipata kumjaribu tena kipa wa Sevilla.

Griezmann aliingia uwanjani kunako dakika ya 76 kujaza pengo la Braithwaite. Hata hivyo, ujio wake haukuathiri hamasa ya Sevilla ambao nusura wapate bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa beki Sergio Reguilon anayewachezea kwa mkopo kutoka Real Madrid.

Barcelona kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Athletic Bilbao mnamo Juni 23, mchuano ambao unatazamiwa kumpa Messi jukwaa la kuwafunga bao lake la 700 katika taaluma ya soka.

Mbali na Sociedad kualika Real, ilikuwa pia zamu ya Celta Vigo kuvaana na Alaves kisha Valencia kupimana ubabe na Osasuna mnamo Juni 21.