Sevilla wamsajili Martial kutoka Man-United kwa mkopo

Sevilla wamsajili Martial kutoka Man-United kwa mkopo

Na MASHIRIKA

SEVILLA wamemsajili mshambuliaji wa Manchester United, Anthony Martial kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu huu na kikosi hicho kitakuwa huru kumpokeza mkataba wa kudumu mwishoni mwa muhula.

Mshahara wote wa Martial utakuwa ukilipwa na Sevilla katika kipindi hicho cha mkopo. Martial, 26, amekuwa akiwaniwa na Sevilla kwa miezi kadhaa tangu alipoanza kusugua benchi kambini mwa Man-United.

Martial alijiunga na Man-United kwa Sh5.6 bilioni mnamo 2015 baada ya kuagana na AS Monaco ya Ufaransa.

Aliwajibikia Man-United kwa mara ya kwanza chini ya kocha Ralf Rangnick mnamo Januari 22, 2021 alipoingia uwanjani katika kipindi cha pili na kusaidia miamba hao kucharaza West Ham United 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Martial amechezea Man-United mara 11 pekee msimu huu na kupachika wavuni bao moja, dhidi ya Everton mnamo Oktoba 2, 2021.

Sevilla wanapigiwa upatu wa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu. Zikisalia mechi 16 pekee katika kipute hicho, Sevilla kwa sasa wanakamata nafasi ya pili jedwalini kwa alama 46, nne pekee nyuma ya viongozi Real Madrid.

Wanasoka wengine wanaotarajiwa kuagana na Man-United mwezi huu ni Jesse Lingard anayehusishwa pakubwa na Newcastle United pamoja na kipa Dean Henderson ambaye ameshindwa kuhimili ushandani mkali kutoka kwa David de Gea.

Muhula mfupi wa usajili wa wanasoka utafungwa rasmi mnamo Januari 31, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kivutha akerwa na naibu wake kuegemea kwa Ruto

Jumwa aponyoka pingu kesi ya uuaji

T L