Sevilla wapepeta Barcelona kwenye mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Copa del Rey

Sevilla wapepeta Barcelona kwenye mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Copa del Rey

Na MASHIRIKA

KIUNGO Ivan Rakitic alifunga bao dhidi ya waajiri wake wa zamani Barcelona na kusaidia kikosi chache cha sasa kusajili ushindi wa 2-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Copa del Rey mnamo Jumatano usiku uwanjani Ramon Sanchez-Pizjuan.

Sevilla walifungua ukurasa wao wa mabo katika dakika ya 25 kupitia kiungo Jules Kounde kabla ya Rakitic kuzamisha kabisa chombo cha Barcelona katika dakika ya 85.

Kounde alikimbia na mpira kutoka ndani ya kijisanduku chao na kuwapiga chenga wanasoka wanne wa Barcelona kabla ya kuwatoka kirahisi mabeki watatu na kumwacha hoi kipa Marc-Andre ter Stegen.

Rakitic aliondoka uwanjani Camp Nou mwishoni mwa Agosti 2020 baada ya kuwaongoza Barcelona kutia kapuni mataji 11 katika mashindano mbalimbali.

Nusura Lionel Messi awafungie Barcelona goli la kuwafutia machozi mwishoni mwa kipindi cha pili ila juhudi zake zikazimwa na kipa Yassine Bono ambaye ni raia wa Morocco.

Chini ya kocha Julen Lopetegui, Sevilla kwa sasa watatua uwanjani Camp Nou kwa mechi ya mkondo wa pili mnamo Machi 3 wakijivunia afueni ya Barcelona kutopata bao la ugenini katika gozi la mkondo wa kwanza.

Barcelona ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Ronald Koeman, waliwahi kuwapepeta Sevilla 5-0 kwenye fainali ya Copa del Rey miaka mitatu iliyopita.

Athletic Bilbao ambao wanapigiwa upatu wa kutwaa taji la Copa del Rey 2019-20 kwenye fainali iliyopanguliwa na kuratibiwa upya kusakatwa Aprili 2021, watakuwa leo wenyeji wa Levante kwenye mkondo wa kwanza wa nusu-fainali za kipute hicho msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Usicheze na Rais – Jenerali

Atalanta yadengua Napoli na kujikatia tiketi ya kuvaana na...