Michezo

Sevilla wapiga Betis 2-0

June 12th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SEVILLA walitandika Real Betis 2-0 katika soka ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyorejelewa Alhamisi ya Juni 11, 2020 baada ya kusitishwa kwa kipindi cha miezi mitatu mnamo Machi 10 kutokana na janga la corona.

Baadhi ya mashabiki waliokongamana kwenye makundi nje ya uwanja wa Ramon Sanchez-Pizjuan walivunja kanuni za afya zilizopo za kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Fowadi Lucas Ariel Ocampo, 25, ambaye ni mzawa wa Argentina ndiye aliyekuwa shujaa wa Sevilla na mchezaji aliyetia fora zaidi katika gozi hilo maarufu jijini Seville.

La Liga ndicho kipute cha pili miongoni mwa Ligi Kuu tano za bara Ulaya kurejelewa baada ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga). Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) inatazamiwa kuanza wiki ijayo huku soka ya Italia ikianza leo kwa nusu-fainali ya Coppa Italia kati ya Juventus na Napoli.

Baada ya kimya cha dakika moja kwa heshima ya walioaga dunia kutokana na janga la corona, kipenga cha kuashiria mwanzo wa La Liga kilipulizwa saa tano kamili usiku wa Juni 11, 2020.

Kelele za mashabiki hai waliorekodiwa katika mechi za awali zilisikika uwanjani kwa umbali sana huku viti katika eneo la mashabiki kukalia vikipakwa rangi za klabu za Sevilla kwa upande mmoja na upande mwingine ukawa na rangi za Real Betis.

Nyuma ya viti kuliandikwa, “Mchezo salama, Utalii salama – Uhispania inakukaribisha”.

Ocampo alishuhudia mojawapo ya makombora yake yakigonga mwamba wa goli la Real Betis katika kipindi cha pili kabla ya kuwafungulia waajiri wake ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penalti kunako dakika ya 56.

Ubunifu wake mkubwa ulimwezesha kumega krosi maridhawa iliyojazwa kimiani na Fernando Reges kunako dakika ya 62.

Barcelona wanaoongoza kilele cha jedwali kwa alama 58 watashuka dimbani hapo kesho dhidi ya Real Mallorca huku Real Madrid wakivaana na Eibar mnamo Jumapili ya Juni 14, 2020.