Michezo

Sevilla watozwa faini kwa kuchelewesha mechi ya Europa League dhidi ya Wolves

August 14th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la soka la bara Ulaya (Uefa) limewatoza Sevilla Sh1.2 milioni kwa kuchelewa kufika uwanjani wakati wa mechi ya robo-fainali ya Europa League iliyowakutanisha na Wolves mnamo Agosti 11, 2020.

Uefa imempa pia kocha Julen Lopetegeui onyo kali kwa kutowajibika vilivyo na kuhakikisha kwamba masogora wake wanafika ugani mapema kwa minajili ya gozi hilo la mkondo mmoja lililosakatiwa mjini Duisburg, Ujerumani. Mechi ilicheleweshwa kwa dakika sita zaidi.

Sevilla ambao ni mabingwa mara tano wa kipute cha Europa League, waliwapokeza Wolves kichapo cha 1-0 katika mechi hiyo iliyomshuhudia fowadi Lucas Ocampos akipachika wavuni goli la pekee na la ushindi.

Ushindi huo wa Sevilla uliwakatia tiketi ya kupepetana na Manchester United kwenye nusu-fainali za Europa League msimu huu mjini Dusseldorf mnamo Agosti 16, 2020. Man-United walisonga mbele kwenye kivumbi hicho baada ya kuwadengua FC Copenhagen ya Denmark kwa bao 1-0 mnamo Agosti 10, 2020 uwanjani MSV Arena, Duisburg.

Inter Milan watakutana na Shakhtar Donetsk kwenye mechi nyingine ya nusu-fainali.