SGR: Jinsi Wachina walivyozima Uhuru

SGR: Jinsi Wachina walivyozima Uhuru

NA PHILIP MUYANGA

RAIS Uhuru Kenyatta alishindwa kutimiza ahadi aliyotoa kwa Wakenya mnamo 2018 kuwa angetoa kwa umma kandarasi kati ya Kenya na China ya ujenzi wa reli ya SGR kwa sababu makubaliano hayo yanahitajika kuwekwa siri kuu.

Katibu wa Wizara ya Uchukuzi, Joseph Njoroge amesema kuwa mikataba iliyowekwa baina ya serikali na wanakandarasi wa kutoka China kuhusiana na ujenzi wa SGR ya Sh450 bilioni uko na vipengele vya kutotoa habari zilizomo kwa umma.

Kupitia hati yake ya kiapo mahakamani, Dkt Njoroge alisema itakuwa ni kukiuka maelewano ya mkataba wa makubaliano iwapo yaliyomo kwenye kandarasi hiyo yatafichuliwa kwa umma.

Katibu wa Wizara ya Uchukuzi, Joseph Njoroge. PICHA | MAKTABA

Mnamo Desemba 29, 2018 akiwa katika Ikulu ya Mombasa, Rais Kenyatta aliambia wanahabari kuwa alikuwa tayari kufichua yaliyomo kwenye kandarasi hiyo kwani haikuwa siri: “Unataka nakala ya kandarasi yenyewe? Rafiki yangu, nitakupatia nakala hiyo kesho.”

Ahadi ya Uhuru kwa Wakenya

Lakini hadi sasa bado hajatimiza ahadi hiyo kwa kile ambacho sasa kimeibuliwa na Dkt Njoroge kuwa akifanya hivyo atakiuka makubaliano ya kuweka siri.

Kwenye kesi ambapo wanaharakati wawili, Bi Wanjiru Gikonyo na Bw Khelef Khalifa, wameenda kortini wakitaka kufichuliwa kwa makubaliano hayo, Dkt Njoroge alisema kandarasi hizo ni baina ya serikali mbili za Kenya na China na kufichuliwa kwake kunaweza kuhatarisha usalama wa kitaifa.

“Baada ya kupata ombi la kutaka habari kutoka kwa waliowasilisha kesi hii, Shirika la Reli nchini lilijibu na kueleza kuwa mikataba ya miradi ambayo wanataka habari kuihusu ni baina ya serikali ya China na serikali ya Kenya,” alisema Dkt Njoroge.

Athari za ufichuzi

Dkt Njoroge alisema iwapo mahakama itakubali ombi la wanaharakati hao, basi hatua hiyo itahatarisha usalama wa kitaifa na kutatiza uhusiano kati ya Kenya na China.

Katibu huyo aliongeza kuwa Bi Gikonyo na Bw Khalifa wameshindwa kuelezea umuhimu wa stakabadhi hiyo kwao na manufaa yake kwa umma iwapo watapewa.

“Wawasilishaji kesi hii wameshindwa kuonyesha umuhimu wa mikataba hii kwao na kwa umma, na hakuna sababu iliyoonyesha kuwa ni hatua gani muhimu watatekeleza iwapo watapewa stakabadhi hizo,” alisema Dkt Njoroge.

Katibu huyo alisema uhuru wa washtakiwa wa kutotoa stakabadhi hizo ni wa kikatiba na umelindwa na sheria ya kupata habari kwa kuwa kuwekwa wazi kwa stakabadhi hizo kunaweza kuhujumu usalama wa taifa.

Dkt Njoroge aliongeza kuwa vipengele katika mkataba huo vinatoa habari kuhusu serikali za nje na vitakuwa na athari kwa usalama wa taifa na uhusiano wa kigeni.

Aliongeza kuwa kuwekwa wazi kwa mikataba hiyo kunaweza kuathiri uwezo wa serikali wa kusimamia uchumi wa nchi iwapo kutakuwa na kukiukwa kwa makubaliano na nchi za nje au mashirika.

Kulingana na kesi ya wanaharakati hao, Bw Khalifa katika barua zake za Desemba 2019 na Mei 2021 aliandikia makatibu wa Wizara ya Uchukuzi na Fedha akiomba nakala za kandarasi baina ya serikali na wote wanaotoa huduma kuhusiana na SGR.

Walisema kuwa stakabadhi kuhusiana na mradi wa SGR pamoja na fedha zilizotumika hazijawekwa wazi kwa umma licha ya kuwa mradi huo uliofanywa na serikali ni wa umma na ni ghali sana.

Wanataka agizo litolewe ya kuwa kutotoa taarifa wanazotaka na kuziweka wazi ni kinyume cha haki ya kupata habari.

Kumekuwa na hofu kuwa baadhi ya vipengele katika kandarasi hizo vina madhara makubwa kwa Kenya kama vile uwezekano wa China kutwaa baadhi ya raslimali kuu za Kenya kama vile bandari ya Mombasa ikiwa Kenya itashindwa kulipa deni ililokopeshwa kujenga SGR.

You can share this post!

Wanajeshi wa Uganda walia kuzidiwa ujanja

GWIJI WA WIKI: Sasha Kenya

T L