Habari Mseto

SGR yakana kuketisha wanafunzi sakafuni

May 13th, 2024 1 min read

NA HILLARY KIMUYU

SHIRIKA la reli nchini limelazimika kutoa taarifa baada ya picha za wanafunzi wakiwa wameketi sakafuni kuenea katika mitandao ya kijamii.

Picha za wanafunzi hao, zilienezwa kwenye mtandao hapo Jumatatu ambapo walikuwa wanarejea shuleni baada ya Rais William Ruto kutangaza kufunguliwa kwa shule nchini.

“Idadi ya wanafunzi waliotumia usafiri wa reli imekuwa kubwa mno kwetu,” ilisema taarifa ya shirika hilo.

“Tunapenda kuwafahamisha wananchi kwamba kutokana na tangazo la serikali la kufungua shule za msingi na sekondari, shirika limepata mahitaji makubwa ya huduma za abiria kati ya Jumapili, Mei 12 na Jumatatu, Mei 13, 2024, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanaotaka kusafiri kurejea shuleni kwa wakati ili kufungua shule,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Shirika hilo liliwashauri wananachi kwamba limeongeza mabogi ya ziada kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi waliolipia mapema kabla ya kuahirishwa kwa tarehe za ufunguzi wa shule.

Waliongeza kuwa wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha hakuna abiria wakiwemo wanafunzi wanaobaki nyuma na wanafunzi wote wanafika salama katika maeneo mbalimbali wanakoenda.