Habari MsetoSiasa

Sh100m: Ouko kuchunguza ziara ya wabunge Amerika

August 15th, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

MKAGUZI Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko amesema afisi yake itachunguza madai ya ufujaji wa fedha za umma kwenye ziara iliyofanywa na wabunge pamoja na madiwani nchini Amerika majuzi.

Kenya ndiyo nchi iliyotuma wajumbe wengi zaidi kwenye Kongamano Kuhusu Hali ya Mabunge (NCSL) mjini Nashville, Tennesee. Ziara hiyo ilimgharimu mlipa ushuru Sh100 milioni.

Hilo linajiri wakati serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imekuwa ikitangaza mikakati ya kupunguza matumizi ya fedha za umma, hasa safari za nchi za nje miongoni mwa maafisa wa serikali.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wajumbe 5,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Kulingana na sheria, mkaguzi ana mamlaka ya kuchunguza asasi yoyote inayodaiwa kufuja fedha za umma na kuandaa ripoti. Mkaguzi pia ana mamlaka kisheria kutoa ripoti yake kwa umma.

Bw Ouko alitoa kauli hiyo jana akihutubu mjini Embu, alikoweka msingi wa ujenzi wa Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ukanda wa Mashariki kwa gharama ya Sh320 milioni.

Alisema kwamba afisi yake imejitolea kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika bila ubadhirifu wowote.

“Fedha za umma lazima zitumiwe ifaavyo. Tutachunguza ikiwa wabunge walifuja fedha hizo kwenye ziara hiyo,” akasema Dkt Ouko, akiongeza kuwa afisi yake itahakikisha kuwa hilo linazingatiwa.

Afisi hiyo imepangiwa kumalizika kufikia Juni mwaka ujao. Alisema kuwa kipindi chake cha kuhudumu kwa miaka minane kitaisha mnamo Agosti 27. Alisema kuwa amefikia mengi licha ya changamoto alizokumbana nazo.

Kulingana na Kipengele 251 cha Katiba, Mkaguzi Mkuu anapaswa kuhudumu kwa kipindi kimoja cha miaka minane.

Gavana wa Embu Martin Wambora alimsifu kwa kumaliza kuandaa ripoti za kifedha za kaunti kwa muda ufaao, lakini akalilaumu Bunge la Kitaifa kwa kuchelewa kuzipitisha kwa muda unaofaa