NA KALUME KAZUNGU
JUMLA ya Sh143 bilioni zimekadiriwa kutumika kwa ujenzi na mpangilio wa miji mikuu mitatu itakayotegemewa kuendeleza biashara kwenye mradi wa Bandari ya Lamu na miundomsingi ya Uchukuzi kutoka Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia (LAPSSET).
Miji hiyo mitatu ni Lamu, Isiolo na ule wa Lokichar ulioko kaunti ya Turkana.
Kulingana na ripoti kutoka kwa Halmashauri ya Ujenzi na Maendeleo ya Lapsset (LCDA), jiji litakalogharimu fedha nyingi zaidi ni Lamu, ambapo Sh114 bilioni zimekadiriwa kutumika.
Jiji la Isiolo linafuata ambapo karibu Sh24 bilioni zimekadiriwa kutumika ilhali Lokichar ikifunga orodha, ambapo karibu Sh5 bilioni zimepangwa kutumika.Akizungumza wakati alipozuru Bandari ya Lamu juma hili, Afisa Mkuu Msimamizi wa LAPSSET, Stephen Ikua alisema majadiliano yanaendelea ili kuona kwamba miradi mingine ya Lapsset ambayo haijatekelezwa, ikiwemo ujenzi wa miji hiyo mikuu inaanza.
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Bandari ya Lamu tayari imekamilika kwani viegesho vitatu vya mizigo kwenye bandari hiyo vimejengwa, kukamilika na hata kuanza shughuli zake.Magati hayo matatu yaligharimu serikali ya kitaifa kima cha Sh49 bilioni kujengwa.
“Tumefurahia kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi wa Bandari ya Lamu imekamilika. Magati matatu ya mizigo bandarini hapa yako chonjo na shughuli za uchukuzi zinaendelea. Kuna viambata vingine vya Lapsset ambavyo pia majadiliano yanaendelea ili ujenzi kuanza, ikiwemo ile miji mikuu mitatu ambayo ni Lamu, Isiolo na Lokichar. Tuko imara kuona kwamba azma hiyo inatimia,” akasema Bw Ikua.