Habari

Sh15 bilioni za mradi wa vipakatalishi vya bure ziliyeyuka – Ouko

October 17th, 2018 1 min read

EDWIN MUTAI NA PETER MBURU

MALIPO ya vocha za Sh15.2 bilioni zilizotumika wakati wa Rais Uhuru Kenyatta kuzindua mradi wa vipakatalishi vya bure kwa shule za msingi hayawezi kupatikana, katika ufichuzi wa Mkaguzi Mkuu Edward Ouko ambao unaibua maswali tele katika mradi huo wa Rais.

Bw Ouko aidha amefichua kuwa Sh603milioni zingine zilitumika kununua vipakatalishi ambavyo vilikuwa na hitilafu vilipotolewa dukani, katika ripoti yake ambayo imelaumu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia (ICT) ambayo ilijukumiwa kutekeleza mradi huo.

Bw Ouko amesema kuwa hitilafu za vifaa hivyo vya kidijitali hazikuwa zimerekebishwa hadi kufikia wakati wa kufanya ukaguzi wake, mnamo Machi, 2018.

Mkaguzi huyo amesema kuwa malipo ya Sh15.2 bilioni kutoka kwa wizara ya ICT hayakudhibitishwa na vocha kama inavyohitajika wakati wa kufanya ukaguzi.

Alisema kuwa mamlaka ya ICT ilitoa barua tisa pekee, kama idhibati ya malipo ya pesa hizo zote.

“Kufuatia hayo, haijawezekana kueleza kwa uhakika namna Sh15,151,069,367 zilitumika,” Bw Ouko akasema kupitia ripoti iliyowasilishwa mbele ya bunge Jumanne.

Hata hivyo, waliosambaza vifaa hivyo vya kidijitali hawajatajwa katika ripoti hiyo.

Alisema kuwa katika nakala zake za mwisho, wizara ya ICT ilisema kuwa kwa jumla ilitumia Sh18.4 bilioni katika programu za vifaa vya kidijitali, vikiwepo vipakatalishi hivyo vilivyokuwa na hitilafu.

“Baada ya kuzindua vipakatalishi hivyo, kamati ya kutekeleza ilizunguka kufanya ukaguzi na kubaini kuwa vyote vilikuwa na hitilafu zilizofaa kutatuliwa na muuzaji. Hata hivyo, hadi wakati wa ukaguzi mnamo Machi 2018, hakukuwa na ushahidi kuonyesha kuwa mashine hizo zilibadilishwa,” Bw Ouko akasema.

Aidha, Bw Ouko ametilia shaka matumizi ya Sh1.6 bilioni kwa programu ya ‘Presidential Digital Talent’ ambayo anasema nakala za kudhibitisha hazikutolewa.