Michezo

Sh2 milioni kwa mshindi wa SportPesa Shield

May 22nd, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WADHAMINI wapya wa Kombe la Ngao (awali GOtv Shield), kampuni ya bahati nasibu ya SportPesa, wametangaza mgao wa tuzo wa makala ya mwaka 2018.

Mshindi atazawadiwa Sh2 milioni. Nambari mbili na tatu watatia mfukoni Sh1 milioni na Sh750, 000, mtawalia. Timu itakayomaliza katika nafasi ya nne itapokea Sh500,000.

SportPesa imetangaza jijini Nairobi kwamba itafadhili mashindano haya kuanzia mwaka 2018 kwa kipindi cha miaka mitatu. Kombe lenyewe sasa litafahamika kama SportPesa Shield.

Makala ya mwaka 2018 yamevutia klabu 64. Timu 13 zinatoka katika Ligi Kuu. Timu hizo ni AFC Leopards, ambayo inatetea taji, Bandari, Tusker, Posta Rangers, Kakamega Homeboyz, Ulinzi Stars, Nzoia Sugar, Vihiga United, SoNy Sugar, Wazito, Kariobangi Sharks, Gor Mahia na Sofapaka.

Klabu tisa zinatoka Ligi ya Supa, 15 ni za Divisheni ya Kwanza, 10 za Divisheni ya Pili na 17 kutoka ligi za matawi.